Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi ya kudhibiti UKIMWI imepungua- UNAIDS

Uchunguzi wa virusi vya HIV
World Bank/Arne Hoel
Uchunguzi wa virusi vya HIV

Kasi ya kudhibiti UKIMWI imepungua- UNAIDS

Afya

Kanda zote ziko nyuma katika kudhibiti kuenea kwa Ukimwi na mafanikio makubwa tuliyopata kwa watoto hayahifadhiwi huku wanawake ndio wanaoathirika zaidi, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI-UNAIDS, Michel Sidibe, wakati wa uzinduzi wa   ripoti mpya ya hali ya UKIMWI duniani hii leo.

Ripoti hiyo imezinduliwa huko Geneva, Uswisi na Paris nchini Ufaransa ambapo Bwana Sidibe amesema rasilimali zilizotengwa haziendani na ahadi za kisiasa zilizopitishwa kukabili Ukimwi na makundi muhimu yanapuuzwa.

Amesema mambo yote hayo yanakwamisha maendeleo na yanahitaji kushughulikiwa haraka.

Ikipatiwa jina, Tumebakiza maili kufika, kuziba mwanya, kutoa mikingamo na kusawazisha kutokuwa na haki, ripoti inasema kuwa maambukizi mapya  ya virusi vya UKIMWI-VVU- yanaongezeka katika mataifa takriban 50, hata na vifo kutokana na UKIMWI havipungui haraka na pia raslimali nazo zinatishia ufanisi.

Maambukizi mapya duniani yamepungua kwa asilimia 18 tu katika kipindi cha miaka saba kutoka  watu milioni2.2 mwaka 2010 hadi milioni 1.8 mwaka 2017.

Katika kinachoonekana kama mgogoro wa kuzuia Ukimwi, ripoti inasema “ijapokuwa idadi hii ni karibu nusu ya maambukizi mapya ikilinganishwa na mwaka wa 1996 ambapo idadi ilikuwa milioni 3.4, bado kasi ya kupungua ni ndogo kuweza kufikia lengo la maambukizi yasiyozidi 500,000 ifikapo mwaka wa 2020.”

Barani Afrika, Nigeria inaonekana kurudi nyuma katika kudhibiti maambukizi mapya huku mtu mmoja tu kati ya watatu wenye VVU ndio wanapata matibabu nchini humo.

Halikadhalika nchini Lesotho, Malawi, Afrika Kusini na Zimbambwe, nusu ya makahaba wana VVU na bado wananyimwa haki ya msingi ya matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Coalition PLUS, Vincent Pelletier amesema jamii zinarudia wito wa UNAIDS za kutaka huduma za kuzuia maambukizi bila ubaguzi.

Ripoti hata hivyo inabainisha ongezeko la uwekezaji wa rasilimali za ndani na nje katika kudhibiti Ukimwi kwenye nchi za kusini na mashariki mwa Afrika ukiambatana na utashi wa kisiasa, ikisema ni dalili kuwa nchi hizo zinaweza kufikia malengo ya mwaka 2020.