“Madiba” akumbukwa kwa uvumilivu wake- Guterres

18 Julai 2018

Leo ni kumbukizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Rais wa kwanza mwafrika wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela.

Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku hiyo imesema inamkumbuka kwa harakati zake za kupigania haki na usawa na zaidi ya yote kuendelea kuleta msukumo duniani kupitia mifano yake wa   ujasiri na huruma.

Katika ujumbe wake wa siku hii inayoadhimishwa tarehe 18 Julai kila mwaka, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres amesema.

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Nelson Mandela alikuwa mateka  kwa miaka mingi, lakini hakuwa mfungwa wa yaliyomfika. Badala yake  alitumia nguvu zake katika kusameheana pamoja na kuona  hali ya baadaye ya   Afrika Kusini yenye amani, makabila tofauti na ya kidemokrasia.”

 

katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi habari katika makao makuu ya UN 12 July 2018
UN Photo/Mark Garten
katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi habari katika makao makuu ya UN 12 July 2018

 Bwana Guterres ameongeza kuwa  ingawa amefariki dunia bado mchango wake unatambulika akisema.

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“ Hakuna mtu ambaye katika historia yake amewahi kufanya mengi kuchochea ndoto za watu wengi na kuwafanya waweke vitendo ndoto zao.Na mapambano ya usawa,heshima  na haki yanaendelea.”

Maadhimisho  ya siku ya leo yaliasisiwa na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  la mwezi Novemba 2009 ambalo lilitangaza siku hii kama ya kimataifa na hiyo ni kutokana na  kazi zake  za kuleta amani na uhuru.

Nelson Mandela wakati huo, wakati huo Naibu Rais wa chama cha African National Congress ANC akiwa  katika ukumbi wa mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN
Nelson Mandela wakati huo, wakati huo Naibu Rais wa chama cha African National Congress ANC akiwa katika ukumbi wa mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 

Mandela akitambulika pia kama Madiba, anakumbukwa kwa kujitolea kwake kutatua migogoro,kuboresha uhusiano baina ya watu wenye asili na rangi tofauti ,kusamehe wengine, kuboresha haki za binadamu, kuendeleza usawa wa kijinsia, kupambana dhidi ya umasikini na mengine mengi.

Watu wengi husherehekea siku hii kwa kufanya kazi za kujitolea kwa dakika sitini na saba, kama vile kufyeka majani sehemu za umma na mambo mengine ya kujitolea.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter