Sahel sio ukanda wa zahma bali wa fursa: Thiaw

Ukanda wa Sahel barani ASfrika haupaswi kuchukuliwa kama ukanda wa zahma, badala yake unapaswa kuonekana kama wa fursa, kwa mujibu wa mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sahel, Ibrahim Thiaw.
Ukanda huo mpana kuanzia Chad katikati mwa Afrika hadi pwani ya Magharibi mwa bara hilo, ni moja ya sehemu masikini wa kupindukia duniani, ambako athari za mabadiliko ya tabia nchi na ugaidi vinaongoza kwa kuongeza hali ya umasikini na kutokuwepo usalama.
Mwezi Juni mwaka huu Umoja wa Mataifa uliwasilisha mawazo mapya ya mpango wa kuurejesha ukanda huo katika msitari unaotakiwa , “Mpango wa msaada wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sahel” ambao unajikita katika nchi 10 zenye jumla ya watu milioni 300 kwa lengo la kuchagiza ukusanyaji wa rasilimali za jamii na uwekezaji wa sekta binafsi. Bwana Thiaw alizuru hivi karibuni ukanda huo na amekiri kweli una changamoto
Nimeshuhudia jamii changa, jamii mahiri zinazofanya kila liwezekanalo kulisha watoto wao, nimewaona wasichana wadogo hawako shuleni, wasichana wadogo wanajifungua katika umri wa miaka 15, miaka 16, ingawa natoka Sahel sijawahi kushuhudia hali hii ya tatizo la ndoa za utotoni ni changamoto kubwa katika sehemu za vijijini hapa Sahel.”
Lakini pia
“Nimeona matumaini, kwa kuwa na nishati mbadala hivi sasa itawezekana kubadili uchumi wa kanda hiyo , kubadili kilimo, kuhifadhi chakula kwa muda mrefu, eneo la Pwani la ukanda huo ni zuri kwa uvuvi, ni ukanda ambao una madini mengi kama mafuta na gesi, hivyo uwezekano upo na fursa zipo ,kitakachohitajika ni mabadiliko, kupewa uzito na jumuiya ya kimataifa kwa upande wa maendeleo na kuwekeza katika maendeleo ya ukanda huo.”
Kwa sasa changamoto za pamoja za ukanda huo amesema ni ukame, mabadiliko ya tabia nchi, uchumi unaoyumba ambao unategemea kilimo cha mvua, pia wanakumbwa na zahma za kibinadamu kila wakati na mabadiliko ya tabia nchi yamezidisha adha.