Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joto latesa zaidi ya watu bilioni moja duniani, maskini taabani- Ripoti

 Pikipiki zenye masanduku  400 ya kupoza joto na kuhifadhia dawa dhidi ya Ebola
UNMEER Photo/Martine Perret Edit
Pikipiki zenye masanduku 400 ya kupoza joto na kuhifadhia dawa dhidi ya Ebola

Joto latesa zaidi ya watu bilioni moja duniani, maskini taabani- Ripoti

Tabianchi na mazingira

Zaidi ya watu bilioni moja duniani wako hatarini kutokana na viwango vya juu vya joto kali na kukosa mbinu za kukabiliana navyo.

Ripoti mpya iliyochapishwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu nishati endelevu kwa wote, SEforALL- imesema viwango vya juu vya joto vinazuia watu wengi  kuondokana na umaskini, husababisha watoto wakose afya nzuri,  ukosefu wa lishe bora n ahata kukosa uchumi wenye tija.

Ikipatiwa jina Matarajio ya kupoza joto; Kupatia fursa endelevu za kupoza joto kwa watu wote,ripoti inasema suala la  uwezo wa kupoza joto ni suala uwiano na kwamba wakati huu ambapo viwango vya juu vimefikia vya juu zaidi,  ina maana ni tofauti kati ya kifo au uhai kwa baadhi ya watu.

Afisa mtendaji mkuu wa shirika hilo ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika suala la nishati endelevu kwa wote, Rachel Kyte amesema katika dunia ambayo inakabiliwa na ongezeko la hali joto, kupata mfumo wa kupoza joto hilo si jambo la anasa bali la muhimu kwa maisha ya kila siku.

Amesema kuwepo kwa hali hiyo ya uhakika ina maana kwamba kuna  uhakika usambazaji vitu vilivyo bora kama vile matunda na vitu vingine, uhifadhi salama wa  chanjo za kuokoa maisha na mazingira salama ya kazi na makazi.

Tutimize mahitaji haya bila kutumia vifaa vinavyoharibu mazingira

Akielezea ripoti kama mbiu ya mgambo, Bi, Kyte amesema ni lazima “tutimize mahitaji haya  bila ya kutumia vifaa vinavyoharibu mazingira, la sivyo kuna hatari dhidi ya  maisha, afya pamoja na dunia tunamoishi,” amesema akiongeza kuwa kwa kufanya hivyo kuna fursa ya kibiashara kwa wale watakaochukua hatua mapema na kukabiliana na hali ya sasa.

Wakati  huo huo, uchambuzi wa mataifa 52 yaliyo katika sehemu za joto unaonyesha kuwa watu milioni 470 wanaoishi kwenye maeneo maskini ya vijijini hawapati chakula salama na matibabu mazuri huku watu wengine milioni 630 katika maeneo maskini na yenye joto mijini wana vifaa duni au hawana kabisa vifaa vya kuwakinga na joto kali.