Ndege zisizo na rubani kudhibiti uvuvi haramu Afrika
"Lengo la teknolojia hiyo si kuondokana na uwepo wa binadamu bali upekee wake ni kwamba inaweza kufanya ufuatiliaji kwenye maeneo ambayo binadamu hawezi kufika na kuamua bila kuingiliwa na mtu yeyote."
Kampuni moja nchini Morocco imeibuka na FishGuard ambayo ni teknolojia ya kutumia ndege zisizo na rubani au drones kudhibiti uvuvi haramu na uporaji wa maliasili barani Afrika.
Badr Idrissi ambaye ni afisa mtendaji wa kampuni hiyo ATLAN Space amesema yeyé na mwasisi mwenza wa kampuni hiyo Younes Moumen walichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa uporaji mkubwa wa masiliasili hizo kuanzia baharini hadi misituni.
“Mathalani tuligundua kuwa Mauritania, Senegal, Gambia, Guinea Bissau, Guinea na Sierra Leone wanapoteza jumla ya takribani dola bilioni 2.3 kila mwaka kutokana na uvuvi haramu,” amesema Bwana Idrissi ambaye aliacha ajira yake kwenye kampuni ya Microsoft ili kuanzisha kampuni hiyo.
Bwana Idrissi amesema walibuni program ambayo inapakizwa kwenye ndege hizo zisizo na rubani, program ambayo inaweza kufuatialia boti ya uvuvi na kubaini iwapo uvuvi unaofanyika ni halali au kinyume cha sheria.
Tuligundua kuwa Mauritania, Senegal, Gambia, Guinea Bissau, Guinea na Sierra Leone wanapoteza jumla ya takribani dola bilioni 2.3 kila mwaka kutokana na uvuvi haramu
“Katika hiyo programu tunakuwa tumeipatia taarifa kuhusu ulinzi wa maeneo ya majini, maeneo yaliyoshamiri zaidi kwa uvuvi haramu pamoja na hali ya hewa. Pia tunaipatia taarifa za kuwezesha kutofautisha mazingira moja na mengine,” amesema Afisa mtendaji mkuu huyo wa ATLAN Space.
Amesema baada ya uchambuzi, ndege hiyo isiyo na rubani ambayo inaweza kukagua eneo la ukubwa wa kilometa 1,000 za mraba huamua iwapo iripoti tukio hilo au la.
“Iwapo itakuwa na uhakika wa asilimia 95 kuwa tukio la uvuvi linalofanyika ni haramu, basi itatuma taarifa kwa mamlaka za eneo husika kuhusu eneo ambako chombo hicho cha uvuvi kinapatikana,” amefafanua.
“Ndege zetu hizi zinaenda eneo kubwa zaidi kwa kuwa zilizopo uwezo wake ni asilimia 70 tu ya eneo hilo, na pia zinapaa hewani kiasi kwamba haziwezi kufikiwa na chombo chochote kisicho cha kijeshi,” amesema Bwana Idrissi.
Amesisitiza kuwa lengo la teknolojia hiyo si kuondokana na uwepo wa binadamu bali upekee wake ni kwamba inaweza kufanya ufuatiliaji kwenye maeneo ambayo binadamu hawezi kufika na kuamua bila kuingiliwa na mtu yeyote.
“Teknolojia yetu zaidi ya yote si ya kuchukua nafasi ya binadamu, la hasha bali inalenga kufanya kazi ya binadamu iwe bora zaidi kwani shughuli haramu zinaharibu ajira,” amesema Bwana Idrissi.
Teknolojia hiyo iendayo kwa jina la FishGuard itaanza kutumika nchini Seychelles na baadaye kuenezwa maeneo mengine huku wakiwa na mpango wa kubuni njia kama hiyo kudhibiti uporaji wa madini na mali za misitu.
Afisa habari wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UN Environment kwa kanda ya Afrika Mohamed Atani akizungumzia teknolojia hiyo amesema ni vyema kusaidia wajasiriamali vijana wa Afrika kwa kuwa wanachangia katika maendeleo endelevu.
Ametoa wito wa kusaka miradi mingi zaidi ya ubunifu kama FishGuard ili kupata suluhisho kwa matatizo yanayokumba bara la Afrika.