Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka umachinga hadi mpishi mkuu katika hoteli ya kifahari

Mpishi kutoka hoteli ya kifahari Thailand na Australia akiwaonjesha wageni vyakula mbalimbali
UNEP Asia Pacific
Mpishi kutoka hoteli ya kifahari Thailand na Australia akiwaonjesha wageni vyakula mbalimbali

Kutoka umachinga hadi mpishi mkuu katika hoteli ya kifahari

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mradi wa mafunzo ya uanagenzi wa  shirika la Umoja wa Mataifa la ajira, ILO, umeanza kuzaa matunda nchini Tanzania na hivyo kuwezesha vijana kukabiliana na changamoto za ajira.

Barnaba Barungi,  mmoja wa wanufaika wa  mradi  huo hakubahatika kupata elimu kutokana na hali duni ya familia yake na hivyo alijikuta akifanya biashara ndogondogo ya kuuza samaki  katika mitaa ya jiji la Dar Es Salaam, nchini Tanzania.

Hata hivyo kupitia mafunzo ya uanagenzi yanayotolewa na ILO, Barungi alisomea upishi na hatimaye  kufanya mafunzo ya vitendo katika hoteli ya Southern Sun  ambayo ni kati ya hoteli za kifahari nchini Tanzania.

ILO kupitia makala iliyochapishwa kwenye wavuti wake inasema kuwa Barungi  baada ya kuhitimu mafunzo ya upishi na kufanya vizuri katika mafunzo kwa vitendo, aliajiriwa na hoteli ya Southern Sun kama mpishi mkuu.

Shirika hilo linasema kuwa bila uanagenzi, fursa ya ajira na mustakabali bora wa maisha kwa vijana kama Barungi husalia njia panda.

Kwa mujibu wa ILO, mafunzo ya aina hiyo hutolewa kwa vijana wengine wengi ambao walihitimu katika programu hiyo ya uanagenzi .

Bwana Ashwani Aggarwal ambaye ni mkufunzi mkuu wa programu ya uanagenzi tangu ianzishwe miaka minne iliyopita  nchini Tanzania amesema, ILO ina mipango ya kupanua mafunzo katika fani za ujenzi, utengenezaji wa ngozi ili kupenya katika soko la  ajira za viwanda nchini humo.

Ni kwa mantiki hiyo katika siku ya leo ya kimataifa ya uanagenzi na stadi za vijana, ILO inatoa wito kwa vijana walioko katika soko la ajira kuhakikisha  kwamba wanapata ujuzi unaoendana na soko la ajira la sasa. 

Halikadhalika shirika hilo limesema kwa kuwa mfumo wa elimu na mafunzo katika  taasisi za elimu hauwahakikishii wanafunzi ujuzi unaohitajiwa na waajiri, uanagenzi ni muhimu zaidi kwa kuwa unawapata vijana  na watu wazima ujuzi huo.

ILO inasema uanagenzi huwezesha vijana kujifunza kwa vitendo mahali halisi  pa kazi na kutumia vifaa vya kisasa, na kuwawezesha wanafunzi kuwa na mkataba unaolinda haki zao na kupata kazi yenye sifa.