Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya raia CAR bado waendelea- Baraza

Mlinda amani wa UN akiwa kwenye doria katika viunga vya mji mkuu wa CAR, Bangui
UN/Eskinder Debebe
Mlinda amani wa UN akiwa kwenye doria katika viunga vya mji mkuu wa CAR, Bangui

Ukatili dhidi ya raia CAR bado waendelea- Baraza

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza masikitiko yake makubwa kutokana na kuendelea kwa ghasia zinazofanywa na vikundi vilivyojihami huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Vikundi hivyo vinaelekeza ghasia hizo dhidi ya raia, walinda amani na wafanyakazi wa misaada kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui pamoja na maeneo mengine ya nchi.


Taarifa ya Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Julai, Balozi Olof Skoog wa Sweden imesema kuwa ghasia hizo ni kinyume cha sheria za kimataifa za binadamu.

Imetaja ukiukwaji huo wa  haki kuwa ni ukatili dhidi ya watoto pamoja na ukatili wa kingono na mateso mengine yanayosababisha idadi ya vifo, majeruhi na ukimbizi wa ndani.

Baraza la Usalama kupitia taarifa hiyo imesisitiza “ kuunga mkono mpango wa bara la Afrika wa amani na maridhiano, CAR, na mwelekeo wa utekelezaji uliopitishwa mjini Libreville, Gabon tarehe 17 mwezi Julai mwaka jana ambavyo kwa pamoja vinaweka mfumo kamili wa suluhu ya kisiasa nchini CAR kama ilivyokubaliwa na mamlaka za nchi hiyo na uongozi wake.”

Ingawa hivyo baraza hilo limetambua hatua zilizochukuliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA pamoja na nchi zinazochangia askari na polisi wa kulinda amani.

Naibu Mkuu wa OCHA Ursula Mueller akizungumza na mwanamke mmoja ambaye alijifungua mwanae njiani wakati akikimbia mapigano kwenye mji wa Paoua nchini humo CAR.
OCHA
Naibu Mkuu wa OCHA Ursula Mueller akizungumza na mwanamke mmoja ambaye alijifungua mwanae njiani wakati akikimbia mapigano kwenye mji wa Paoua nchini humo CAR.

Wajumbe wamesema MINUSCA na watendaji hao wamesaidia kukabiliana na ukatili na unyanyasaji wa kingono.

Hata hivyo bado wameonyesha wasiwasi wao juu ya vitendo hivyo vya ukatili wa kingono vinavyofanywa na walinda amani na watendaji wasio wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

“Tunasisitiza umuhimu wan chi zinazochangia askari na polisi, MINUSCA kuchunguza haraka madai ya ukatili wa kingono kwa njia halali na ya uwazi ili wahusika waweze kufikishwa mbele ya sheria na kuwajibika,” imesema taarifa hiyo.

Kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini humo wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema si nzuri kwa kuwa karibu nusu ya idadi ya watu CAR wanahitaji misaada ya kibinadamu.

“Tunaomba pande zote husika kwenye mzozo ziruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie walengwa bila vikwazo vyovyote,” imesema taarifa hiyo ikimalizia kwa kuongeza kuzisihi  nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziongeze usaidizi wao wa kifedha ili kukidhi mahitaji yaliyoainishwa kwenye mpango wa usaidizi wa kibinadamu wa CAR kwa mwaka 2018.

TAGS: CAR, Baraza la Usalama, Usalama,