Nchi za kiarabu anzisheni mifumo jumuishi ili kupata maendeleo- IMF

Wito huo umetolewa leo mjini Beirut Lebanon na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya kati na Asia ya kati katika shirika la fedha duniani -IMF Jihad Azour kwenye mkutano wa kiuchumi wa mataifa ya kiarabu.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa eneo la uarabuni ndilo lenye idadi kubwa ya vijana wasio na ajira duniani akisema kuwa vijana zaidi ya milioni 27 watakuwa wakitafuta kazi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa, mabadiliko katika mifumo inayosaidia ukuaji jumuishi yanaweza kusaidia kuleta mafanikio makubwa.
Bwana Azour ametaja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kusaidia makundi yaliyotengwa au yaliyo pembezoni ili yaweze kuwa sehemu ya uchumi. Kwa mantiki hiyo amesema sera ni lazima ziridhiwe ili kujumuisha vijana, wanawake na wakazi wa vijijini kwenye nguvu kazi ya taifa kwa kuwaandaa kwa kazi zinazofaa.
“Ujumuishi wa kifedha ikiwemo matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha ni mbinu muhimu ya kuwezesha raia kwa kuwa takribani asilimia 70 ya wakazi wa ukanda huo wa mashariki ya kati na Asia ya Kati hawana akaunti za benki,” amesema Bwana Azour.
Hatua nyingine kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa IMF ni kutunga sera za fedha zinazowekeza katika rasilimali watu na miundombinu.
Amesema hatua hiyo inawezekana iwapo sera hizo za fedha zitabuniwa upya ili kuhakikishe makusanyo yote ya fedha za umma yanatumika kuboresha miundombinu ya kijamii ikiwemo elimu, afya, huduma za pensheni na barabara.
Amewasifu vijana wa eneo hilo akisema wana vipaji na iwapo watapewa wanafasi watadhihirisha umuhimu wa kukuza uchumi jumuishi kwa mafanikio ya muda mrefu ya kanda hiyo.
Bwana Azour, amesema kuwa IMF inaamini kuwa jamii huimarika ikiwa kila mmoja wake atapata nafasi na ndio maana ni muhimu kwa nchi za kanda ya kiarabu kuwekeza katika vijana wenye vipaji na kutumia vema nafasi za mawasiliano kuwasiliana na maeneo mengine ya dunia.