Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maganda ya vyakula yageuzwa mkaa nchini Kenya

Chebet Lesan, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bright Green Renewable Energy, shirika linalohusika na kutengeneza makaa  yatokanayo na maganda ya vyakula nchini  Kenya, akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.
UN News/Assumpta Massoi
Chebet Lesan, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bright Green Renewable Energy, shirika linalohusika na kutengeneza makaa yatokanayo na maganda ya vyakula nchini Kenya, akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya UN jijini New York, Marekani.

Maganda ya vyakula yageuzwa mkaa nchini Kenya

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno! ni usemi ambao unadhihirika hivi sasa nchini  Kenya ambako shirika moja linatumia maganda ya mazao kutengeneza nishati ambayo ni mkombozi hasa kwa wanawake ambao macho yao hugeuka kuwa mekundu na kudhaniwa kuwa ni wachawi kutokana na moshi wa kuni na mkaa utokanao na miti.

Nchini Kenya teknolojia ya kubadilisha maganda ya kahawa, miwa na mahindi kuwa nishati safi ya mkaa wa kupikia imeleta nuru siyo tu kwa wanawake bali pia kwa watu ambao awali walikuwa hawana mahali pa kutupa taka hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Bright Green Renewable Energy Chebet Lesan amesema hayo akihojiwa na Idhaa hii kando mwa jukwaa la ngazi ya juu linalotathmini utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs jijini New York, Marekani, akifafanua vile ambavyo wanatengeneza.

Amesema "tunachukua maganda ya miwa, mahindi na kahawa ambayo watu wanataka kutupa. Kisha tunayachoma kama vile ambavyo watu huchoma magogo na miti ili kupata mkaa. Hatimaye baada  ya kuchomwa maganda hayo hugeuka unga laini ambao hubinywa na kugeuzwa vitofali vidogo. Vitofali hivyo ndio tunatumia kama mkaa." Amesema Bi. Lesan.

Moshi hubakia historia katika mkaa unaotengenezwa kwa kutumia maganda ya mazao kama vile muwa, kahawa na mahindi
UNICEF/Tanya Bindra
Moshi hubakia historia katika mkaa unaotengenezwa kwa kutumia maganda ya mazao kama vile muwa, kahawa na mahindi

Bi. Chebet ambaye alijifunza teknolojia hiyo mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania anasema hivi sasa wanauza mkaa akitaja faida zake kuwa ni pamoja na kwamba mkaa huo hauna moshi na zaidi ya yote unaweza kutumia kiasi kidogo kwa mapishi ya siku nzima. Faida nyingine ametaja kuwa ni kwamba mkaa huo unaweza kuuzima unapomaliza kupika na baadaye kuuwasha tena ili kuendelea kupika.

Mradi huu unaenda sambamba na lengo namba 7 la malengo ya maendeleo endelevu ambalo linataka  kuhakikisha kwamba kila mtu kwenye sayari hii ya dunia anaweza kupata nishati ya kisasa na endelevu kwa bei rahisi na kwa uhakika.

Bi Chebet ambaye pia ni muasisi wa shirika hilo amesema anaona furaha zaidi kuweza kubadilisha maisha ya watu hususan wanawake kwa kuwa wao hutumia wanawake wenye vioski kusambaza bidhaa hiyo hadi mashinani.

Kwa mujibu wa Bi. Chebet, kilo moja ya mkaa huo ambao hutosha kupika mlo wa asubuhi, mchana na jioni kwa familia moja hugharimu dola senti 30.