Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unaweza kupora gari au nyumba lakini si elimu ya mtu- Shearer

Mtoto huyu mwenye umri wa miaka 15 akishuhudia tukio la watoto huko Yambio wakirejeshwa kwenye jamii baada ya kutumikishwa vitani. Sasa Chuo cha ualimu kinaleta nuru kwa watoto hawa.
UNICEF/UN0202136/Rich
Mtoto huyu mwenye umri wa miaka 15 akishuhudia tukio la watoto huko Yambio wakirejeshwa kwenye jamii baada ya kutumikishwa vitani. Sasa Chuo cha ualimu kinaleta nuru kwa watoto hawa.

Unaweza kupora gari au nyumba lakini si elimu ya mtu- Shearer

Utamaduni na Elimu

Vita nchini Sudan Kusini vilianza mwezi Disemba mwaka 2013 na hadi hii leo bado kuna mapigano hususan kwenye jimbo la Upper Nile. Ingawa hivyo shirika moja la kujitolea limeamua kuleta nuru kwa vijana na watoto wa eneo hilo kwa kuanzisha chuo cha ualimu.

Nchini Sudan  Kusini, chuo ya ualimu kilichoanzishwa kwenye eneo linalokabiliwa na ghasia kinasaidia kuelimisha na kuponya majeraha kwa vijana ili nao pia waweze kusaidia kizazi kijacho. Siraj Kalyango na maelezo zaidi.

Ni kwenye mji wa Yambio jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, wakurufunzi wa ualimu, wake kwa waume, wakiwa wamevalia sare zao wanamlaki mgeni.

Mgeni ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo David Shearer ambaye amefika eneo hilo kuona jinsi shirika la kiraia la Solidarity South Sudan au mshikamano Sudan Kusini linavyofundisha walimu.

Hadi sasa walimu wapya wapatao 200 wamehitimu kwenye chuo hiki, katika nchi hii ambayo walimu wengi hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa, lakini wakurufunzi hawa vijana wana ari kubwa ya kuwapatia watoto zawadi ya elimu baada ya machungu mengi.

Image
UN Photo/JC McIlwaine
Wanafunzi Sudan Kusini (maktaba). Picha:

Sista Margaret Scott ni mwakilishi wa shirika la Solidarity South Sudan.

 “Kwao huu ni kama wito na si kazi. Ni wito wanaamini na wanatekeleza. Wanataka kusaidia watu. Kila mara wanazungumzia kusaidia vijana na nadhani huu ni mtazamo mzuri kwa elimu.”

Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa ncihni Sudan Kusini aliwahi kuwa mwalimu na ndipo akafunguka..

 “Pindi unapoona bashasha kwa watoto hawa, unaona kabisa wanaona mustakhbali wa nchi  yao. Huwezi kufanya jambo lingine bora zaidi kuliko kuelimisha watu. Unaweza kupoteza nyumba, au gari lakini katu huwezi kuchukua elimu.”

Umoja wa Mataifa unasema katika maeneo mengi ya Sudan Kusini, vijana wanapigana kwa misingi ya tofauti za makabila  yao lakini kupitia shirika hili, vijana wa Yambio wameungana kwa nia moja ya kujifunza na kubadilisha ufahamu.