Warohingya ni waathirika wa maangamizi ya kikabila, na dunia imewaangusha:Guterres

11 Julai 2018

“Watoto wadogo waliuawa mbele ya wazazi wao, wasichana na wanawake waliobakwa kwa pamoja waliteswa na kuuawa na familia zao na vijiji vyao kuchomwa moto.”

Hizi ni baadhi ya shuhuda ambazo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizisikia moja kwa moja kutoka kwa mashahidi na manusura wa kabila la Rohingya alipowatembelea kwenye jimbo la Cox-Bazaar nchini Bangladesh.

Katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la The Washington Post, Antonio Guterres amesema hakukuwa na lolote la kumuandaa kusikiliza shuhuda hizo kutoka kwa wakimbizi wa Rohingya ambao walizihama nyumba zao kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar kuepuka mauaji na machafuko.

 

UNHCR/Patrick Brown
Msichana mkimbizi akiwa amesimama nje kwenye mvua katika kambi ya Shamlapur, Cox's Bazaar

Kuna mwanaume aliyezirahi kwa kulia mbela ya Guterres akielezea jinsi walivyomuua mtoto wake mkubwa wa kiume kwa kumpiga risasi akishuhudia kwa macho yake. Mama mzazi wa mwanaume huyo aliuawa kikatili na nyumba yake kuteketezwa kwa moto.

Guterres amesema , mwanaume huyo alijificha msikitini , lakini askari wakampata, wakamtesa na kuchoma moto Koran.

Guterres ameongeza kuwa shuhuda za kutia machungu za wakimbizi wa Rohingya zitasalia naye daima.

"Waathirika wa kile kinachoolezwa kama ni uangamizaji wa kabila la Rohingya la walio wachache ambao kwa asilimia kubwa ni Waislam, wanakabiliwa na madhila ambayo ynagadhibisha au kumuumiza anayewatembelea “ameongeza bwana Guterres. Ukatili wa kutisha walioupitia umewapa changamoto ya uwezo unaotakiwa kuzingatiwa, lakini ukatili huo ni hali halisi kwa wakimbizi milioni moja wa Rohingya.

 

UNFPA Bangladesh/Allison Joyce
Mhudumu wa afya akitoa huduma kwa mkimbizi mjamzito katika kituo cha afya katika kambi ya wamkimbizi Nayapara

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Warohingya wameteseka sana na kunyimwa haki zao za msingi za binadamu , kuanzia haki ya utaifa kutoka nchini mwao Myanmar.

Ameongeza kuwa ukiukaji wa makusudi wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama nchini Myanmar katika mwaka mmoja uliopita ulikuwa ni wa kuwatia mshikemshike jamii ya Warohingya, na kuwaacha na mtihani mkubwa wa ama kuchagua kusalia nchini humo kwa hofu kubwa ya kuuawa, au kukimbia kuokoa Maisha yao na kuacha kila kitu.

Baada ya safari ndefu kufikia usalama, wakimbizi wa Rohingya sasa wanajaribu kumudu mazingira magumu kwenye jimbo la Cox’s Bazaar nchini Bangladesh ambayo yamesababisha mtafaruku mkubwa kabisa wa wakimbizi duniani.

Guterres amesema “ Bangladesh ni taifa linaloendelea likiwa na shinikizo kubwa la rasilimali zake, na wakati mataifa makubwa na Tajiri duniani yakiwafungia milango wataalam, watu na serikali ya Bangladesh wamefungua mipaka na mioyo yao kwa wakimbizi wa Rohingya.”

 

IOM 2018
Miundombinu ya kudumu itakuwa fursa kubwa kuzuia athari mpya za majanga

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa huruma na ukaribu wa watu wa Bangladesh unadhihirisha utu halisi na bora, kwa kuokoa Maisha ya maelfu ya watu, kalini kukabiliana na mgogoro huu ni lazima kuwe ni kimataifa.

Akisisitiza kuwa mgogoro huu hauwezi kutatuliwa kwa usiku mmoja, lakini hautotakiwa kuendelea milele. Amesisitiza pia umuhimu wa Myanmar kuweka mazingira stahiki ya wakimbizi hao kurejea nyumbani na kuwaahidi Maisha ya amani na utu. Amesema na hilo litahitaji uwekezaji mkubwa katika ujenzi mpya na maendeleo ya jamii zote za moja ya majimbo masikini kabisa Myanmar, lakini pia katika masuala ya upatanishi na kuheshimu haki za binadamu.

Amesema bila kushughulikia mizizi ya machafuko katika jimbo la Rhakhine kikamilifu, zahma na chuki vitaendelea kuwa chachu ya vita, akihimiza kwamba Warohingya hawapaswi kuwa waathirika waliosahaulika.” Ni lazima tushughulikie ombi la warohingya kwa kuchukua hatua” amehitimisha Guterres. 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter