Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya hakikisha sekta ya biashara inazingatia haki za binadamu- Wataalam 

Ukuaji wa kilimo cha kibiashara unaweza kuwa na madhara kwa wafanyakazi iwapo haki za binadamu zitapuuzwa
Benki ya Dunia/Flore de Preneuf
Ukuaji wa kilimo cha kibiashara unaweza kuwa na madhara kwa wafanyakazi iwapo haki za binadamu zitapuuzwa

Kenya hakikisha sekta ya biashara inazingatia haki za binadamu- Wataalam 

Haki za binadamu

Kikundi kazi cha wataalam wa Umoja wa Mataifa juu ya biashara na haki za binadamu kimehimiza mamlaka nchini Kenya kutekeleza kwa vitendo mapendekezo yaliyotajwa katika Katiba ya nchi hiyo ya 2010 ya kuhakikisha biashara zinaheshimu haki za binadamu.

Akihojiwa na Idhaa hii kutoka mjini Nairobi, Kenya mwishoni mwa ziara yake ya siku 10 nchini humo, mwenyekiti wa kikundi hicho  Anita Ramasastry amesema Kenya ina msingi mzuri wa mfumo mzuri wa kisheria kwa ajili ya kulinda haki na hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha utekelezaji wake.

Amesema wakati wa ziara hiyo, wataalam walikutana na wawakilishi wa Serikali, biashara, na mashirika ya kiraia, kujadili fursa na changamoto za kutekeleza Kanuni Ongozi za Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu.

Bi. Ramasastry amesema walitembelea maeneo ya mashambani na kusikitishwa na mazingira magumu yanayokabili wafanyakazi wa mashambani, ambao mara nyingi hulipwa mshahara mdogo na pia walizuru bwawa la maji la Solai ambalo kingo zake zilipasuka na kuleta madhara.

“Kutoka maeneo kama Turkana, Solai, Mombasa ambako jamii kwa kweli wanaathiriwa na shughuli za biashara zilizoanzishwa ambazo zinaleta madhara. Na serikali siyo tu ichukue hatua kuhakikisha inalinda raia lakini hata wafanyabiashara wanapaswa kuwajibika kwa shughuli zao za biashara na madhara yake kwa wafanyakazi bali pia kwa jamii.”

Pia wamekuwa na wasiwasi sana na jinsi madini ya risasi yanaharibu mazingira ya makazi ya Owino Uhuro huko Mombasa, vitendo ambavyo vinaathiri zaidi watu maskini zaidi katika jamii. 

Bi. Ramasastry amesema na iwapo waheshimu haki za binadamu katika mienendo ya biashara

“Watakuwa wameweka mazingira bora kwa uwekezaji Kenya na pia mazingira thabiti kwa eneo la kazi lenye afya na fanisi.”

Katika taarifa yao wataalam hao wamebainisha kuwa changamoto zilizopo zitahitaji hatua halisi ya serikali kuu na mitaa, ikiwa ni pamoja na hatua za kuhakikisha majadiliano na uwazi unaofaa katika tathmini ya athari za mazingira na kijamii ya miradi ya biashara .

Wataalamu pia wamehimiza serikali iendeleze kanuni zinazohusiana na usajili wa ardhi ya jamii na jitihada nyingine za kutoa ufafanuzi wa haki za ardhi na uhakika kwa jamii na sekta binafsi.

"Tunakaribisha ahadi ya serikali ya kuandaa Mpango wa Taifa wa utekelezaji (NAP) juu ya Biashara na Haki za Binadamu ili kushughulikia mapengo na changamoto za sasa na tunatarajia kuwa uchunguzi wetu wa awali utasaidia mchakato huu," Bi. Ramasastry alihitimisha.

Ripoti ya mwisho ya Kundi la Kazi hilo ikiwa ni pamoja na matokeo na mapendekezo muhimu, itawasilishwa kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Juni mwaka 2019.