WMO yazungumzia kuokolewa kwa vijana kutoka pangoni Thailand

10 Julai 2018

Wataalamu wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wamesema mvua za kuambatana na radiambazo zilitabiriwa kunyesha  kaskazini mwa Thailand hazikuzuia juhudi za uokozi wa timu ya wavulana ya mpira wa miguu ambayo ilikwama ndani ya pango kwa kipindi cha zaidi ya wiki mbili.

Msemaji wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani-WMO, Clare Nullis, amesema hayo leo Jumanne  mjini Geneva Uswisi, wakati kukiwa na taarifa kuwa  wavulana wote 12 pamoja na kocha wao  wameokolewa kutoka kwenye pango hilo na kundi la  wapiga mbizi maalum wa kimataifa.

“Walichofanya ni kitu cha kusifika sana hadi sasa na wakuu nchini Thailand nao wameshirikiana vizuri," amesema msemaji wa WMO.

 Kuhusu hali ya hewa eneo hilo amesema kuwa wakati huu ndio mwanzo wa msimu wa mvua za pepo za monsuni nchini Thailand, akiongeza kuwa  “nimekuwa nikifuatilia utabiri wa hali ya hewa kwa  eneo la Chiang-Rai kwa kipindi cha wiki moja na kila siku imekuwa ikionyesha ishara ya kuwepo kwa   mvua kali,” amesema akiongeza kuwa lakini leo kwa bahati nzuri mvua hazikunyesha kama ilivyokuwa inatabiriwa.

Mafuriko yaliua watu 150 Japan

Bi. Nullis amezungumzia pia hali ya hewa kwingineko akisema kuwa kulitokea mafuriko nchini Japan ambayo yalisababisha vifo vya watu 150 huku nyumba takriban 10,000 zikiharibiwa.

Ametaja pia visiwa vya Ryukyu vilivyoko kusini magharibi mwa nchi hiyo ambavyo amesema vimeshambuliwa na kimbunga Maria na kukifanya kisiwa kingine cha Taiwan huko Asia kuwa katika hali ya tahadhari kikijiandaa kupiga jumatano.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter