Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu ya SPLA dhidi ya tukio la hoteli ya Terrain itangazwe:Patten

Jeshi la SPLA Sudan Kusini. Picha:IRIN/Hannah McNeish

Hukumu ya SPLA dhidi ya tukio la hoteli ya Terrain itangazwe:Patten

Haki za binadamu

Pramila Patten, msaidizi wa Katibu Mkuu na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo, leo ametoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini kutangaza hukumu ya kesi inayohusiana na tukio lililofanyika  kwenye hoteli ya Terrain .

Julai 2016 genge la askari wa kundi la SPLA walishutumiwa kuwabaka raia wa kigeni kwenye hotel ya Terrain nchini Sudan Kusini na kumuua mwandishi mmoja wa habari raia wa Sudan Kusini na kesi dhidi yao ilifunguliwa.

Sasa Bi. Patten anasema hukumu dhidi ya kesi hiyo ni muhimu sana kwa kuhakikisha uwajibikaji wa vitendo kama hivyo vinavyokiuka haki za binadamu na utu, kwa wote waliohusika.

Ameongeza kuwa ofisi yake iko tayari kutoa mafunzo ya kiufundi kwa maafisa wanaohusika na mchakato wa kesi hiyo mahakamani, kwa polisi, kwa waendesha mashitaka, kwa wapelelezi, mahakimu, mahakama za kijeshi na kwa mahakama za kiraia.

Amesisitiza kwamba ili kuhakikisha vitendo vya ubakaji vinakomeshwa ni lazima kuwafikisha kwenye mkono wa sheria wahusika na kuwanawajibisha ili iwe funzo kwa wengine, lakini pia kutenda haki kwa waathirika wote na jamii zao.


TAGS: Pramila Patten, Sudan Kusini, SPLA, Terrain Hotel, ubakaji