Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muda wa maneno umekwisha tuchukue hatua tuokoe wanawake- Bi. Mohammed

Mama akimlisha mwanae tikiti maji huko Niamey, mji mkuu wa Niger ambako wanawake wanakumbwa na madhila ikiwemo mila potofu.
UNICEF/Giacomo Pirozzi Edit
Mama akimlisha mwanae tikiti maji huko Niamey, mji mkuu wa Niger ambako wanawake wanakumbwa na madhila ikiwemo mila potofu.

Muda wa maneno umekwisha tuchukue hatua tuokoe wanawake- Bi. Mohammed

Amani na Usalama

Baada ya ziara yao kwenye nchi za Sudan Kusini, Chad na Niger, viongozi wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, leo wamewasilisha ripoti zao mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa kikao kuhusu wanawake, amani na usalama barani humo.

Tuache maneno mengi na sasa tutekeleze kwa vitendo sera, mifumo na ajenda tulizo nazo kuhusu wanawake, amani na usalama, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la umoja huo jijini New York, Marekani.

Kauli yake hiyo inafuatia kile alichoshuhudia wakati wa ziara yake ya pamoja na ujumbe wa Muungano wa Afrika, AU huko Sudan Kusini, Chad na Niger hivi karibuni akisema ingawa wanawake wanakabiliwa na madhila makubwa ikiwemo ukatili wa kingono na shida za kiuchumi, bado wanaweza kuwa mawakala wa mipango mipya na muhimu ya kuwaletea nuru kwenye jamii zao.

“Kwa miaka 18, Baraza hili limekuwa likijadili ajenda ya wanawake, amani na usalama kila mwaka. Kila mara moja kwa mwaka tunasisitizia kuwa usawa wa kijinsia ni msingi wa utulivu na amani. Lakini mara chache sana tumesonga mbele zaidi ya misingi. Sasa ni wakati wa kusonga kutoka kwenye miundo kwenda kwenye vitendo,” amesema Bi. Mohammed.

Ameongeza kuwa kuwekeza kwenye amani hivi sasa kwenye eneo hilo kutakuwa na manufaa kwa dunia nzima.

Bol  nchini Chad, wakati wa ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed (kushoto) akizungumza na Halima Yakoy Adam ambaye ni manusura wa shambulio alilopangiwa kufanya na Boko Haram
UN News/Daniel Dickinson
Bol nchini Chad, wakati wa ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed (kushoto) akizungumza na Halima Yakoy Adam ambaye ni manusura wa shambulio alilopangiwa kufanya na Boko Haram

Naibu Katibu Mkuu amesema azimio namba 1325 na mengine saba yaliyofuatia ni ahadi tosha hivyo “hebu na tuzipatie uhai mbinu hizi na kuhamasisha uhusiano wa karibu zaidi baina ya mpango wa usaidizi wa Sahel, ajenda 2030, ajenda 2063 ya AU na mipango ya kitaifa,” amesema.

Kuwekeza kwenye amani hivi sasa kwenye eneo hilo kutakuwa na manufaa kwa dunia nzima.

Amewakumbusha wajumbe wa Baraza hilo la Usalama kuwa gharama ya kutochukua hatua ni kubwa sana akiongeza kuwa umaskini, taasisi dhaifu na ukosefu wa usawa wa kijinsia ikiwemo mila potofu kama vile ndoa katika umri mdogo ni vichocheo vya misimamo mikali.

Katika ziara hiyo ya nchi tatu za Afrika, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed aliongoza ujumbe huo akiambatana na mjumbe maalum wa AU kuhusu wanawake, amani na usalama Bineta Diop.

Viongozi wengine waliombatana naye ni Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Wallström.