Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hadi leo nakumbuka vilio vya wanawake wakililia watoto wao Aleppo: Shaker

Mtoto huyu akiwa katika moja ya maeneo ya hifadhi ya muda kutokana na mapigano huko mji wa Aleppo nchini Syria.
UNICEF/Khuder Al-Issa
Mtoto huyu akiwa katika moja ya maeneo ya hifadhi ya muda kutokana na mapigano huko mji wa Aleppo nchini Syria.

Hadi leo nakumbuka vilio vya wanawake wakililia watoto wao Aleppo: Shaker

Amani na Usalama

“Muziki uliokoa maisha yangu” kauli hiyo yenye matumaini na yenye lengo la kuwahamasisha wakimbizi wanaopitia  zahma mbalimbali duniani ni kutoka kwa Mariela Shaker mkimbizi kutoka Syria aliyepata bahati ya kipekee ya kusoma kusoma katika chuo kikuu cha muziki  cha Monmouth, Illinois Marekani. 

Bi. Shaker ambaye ni mtaalamu wa kupiga fidla amesema hayo wakati akizungumza katika hafla ya mwaka ya wabunifu wa masuala ya kijamii inayofanyika kila mwaka huko bonde la ubunifu la Silicon jijini San Fransisco nchini Marekani.

Kumbukumbu zikamjia za madhila yaliyomkuta siku ya shambulio lililowauwa zaidi ya wanafunzi 82 katika chuo cha Aleppo nchini Syria mwaka 2011...

Sauti ya Mariela Shaker

“Nikuwa  chuoni nikifuatilia diploma yangu sijui ilikuwaje mpaka nikatoka hapo nikiwa mzima siku hiyo. Hadi  leo hii bado nasikia zile sauti za magari ya wagonjwa mahututi na wanawake wakililia watoto wao.”

Baada ya miezi sita Bi. Shaker alianza yakutafuta wafadhili wa kumsadia kupata chuo nje ya Syria ili aweze kuendelea na shahada ya masomo yake ya muziki.

Sauti ya Mariela Shaker

“Kifo hakikunitishia bali kushuhudia  ndoto zangu zikipotea ndicho kilichonitishia sana. Wiki iliyofuata nilikuwa nahangaika katika vibanda vya iataneti huku nikikoswakoswa na makombora , kwasababu nilidhamiria kutuma maombi katika vyuo mbalimbali duniani ili kupata nafasi ya masomo.”

Kama wasemavyo wahenga mvumilivu hula mbivu, maombi yake yalikubaliwa na chuo kikuu cha sanaa cha Monmouth nchini Marekani ambapo alilipiwa karo yote.

Licha ya vipingamizi vya njiani na kufika Marekani, Bi Shaker alifanikiwa kumaliza masomo yake na kupewa hifadhi ya ukimbzi Marekani ambapo amekuwa anatumia muziki wake kuunga mkono shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR za kuhamasisha wakimbizi.

Sauti ya Mariela Shaker

“Nashukuru kwa nafasi hii ya kipekee ambayo nimepewa kutumbuiza na pia uhamasishaji katika hafla kwa niaba  wanafunzi na wakimbizi wa Syria katika ukumbi wa Kennedy, Chuo Kikuu cha Havard, taasisi ya teknolojia ya Massachussetts, MIT na sehemu zingine mbalimbali.”