Idadi ya wahamiaji wanaorejea kwa hiari nyumbani yapungua- IOM

10 Julai 2018

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM mwaka jana liliwezesha wahamiaji 72,176 kurejea nyumbani kwa hiari na wengine kujumuishwa katika jamii ugenini.

Ripoti ya IOM kuhusu urejeaji nyumbani na ujumuishwaji ugenini ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa kiwango hicho ni pungufu kwa asilimia 27 ikilinganishwa na wahamiaji 98,403 waliorejea nyumbani kwa hiari mwaka uliotangulia.

Msemaji wa IOM mjini Geneva Uswisi, Joel Millman amesema ingawa idadi imepungua kutokana na kutokuwepo kwa idadi kubwa ya wanaotaka kurejea nyumbani kutoka ukanda wa kiuchumi wa Ulaya, EEA na Uswisi bado idadi ya wanufaika wa miradi ya uasidizi baada ya kurejea nyumbani ilikuwa ni kubwa.

Wanufaika wa mradi huo uliopatiwa jina la AVRR walirejea kutoka nchi 124 na kujumuika kwenye nchi 165.

Millman amesema Ujerumani imesalia kuwa nchi inayoongoza kwa kupokea wahamiaji hao ikiwa na asilimia 40 ya wote waliojumuishwa huku Albania ikiwa ni nchi ambayo wahamiaji wamerejea nyumbani kutoka ugenini.

Takwimu zinaonyesha kuwa takribani theluthi moja ya wahamiaji hao waliosaidiwa na IOM ni wanawake na asilimia 25 ni watoto.

IOM inasema kuwa miongoni mwa waliosaidiwa kupitia mpango huo, 3,331 walikuwa hatarini ikiwemo wenye mahitaji ya afya, wahanga wa usafirishaji haramu na watoto wanaosafiri peke yao.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter