Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yashikamana na Msumbiji kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji

Piassa anafanya kazi katika karakana ya baba yake baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa UNIDO. Wahamiaji wanapokuja wanaonekana kama wanapokonya kazi za wenyeji kama hizi
UNIDO
Piassa anafanya kazi katika karakana ya baba yake baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa UNIDO. Wahamiaji wanapokuja wanaonekana kama wanapokonya kazi za wenyeji kama hizi

UN yashikamana na Msumbiji kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la wahamiaji IOM, la kazi ILO na ofisi ya Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa yameshikama na serikali ya Msumbiji kuhakikisha ulinzi kwa wafanyakazi wahamiaji.

Lengo la mshikamano huo ni kuboresha uwezo wa serikali ya Msumbiji kuripoti na pia kutoa msaada wa muuongozo wa kiufundi ili kutekeleza mkataba wa kimataifa wa kulinda haki za wafanyakazi wote wahamiaji na familia zao (CMW) nchini Msumbiji.

Mashirika hayo yameanzisha mafunzo ya kutoa tarifa na warsha maalumu ya kuwashirikisha na kuwajumuisha wahamiaji, ili kuimarisha uwezo wa serikali kutathimini sheria zake, será na mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya kuwasaidia na kuwatendea haki wahamiaji nchini humo.

Mafunzo na warsha hiyo ya siku nne vinakwenda sanjari na viwango vya mkataba wa kimataifa wa wahamiaji wenye lengo la kukomesha michakato inayotoa mwanya wa  kuwanyanyasa na kuwatumia wahamiaji wakati wa shughuli ya kuwajumuisha katika masuala ya kazi.

Msumbiji ni taifa ambalo hivi sasa linashuhudia wimbi la wahamiaji kutoka Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika na imekuwa ni makazi, kituo cha muda na mapokezi ya wahamiaji mchanganyiko, na kutokana na wahamiaji hao kushindwa kuongea lugha ya asili ya nchi hiyo, hali yao ya uhamiaji na kutofahamu vizuri mazingira ya taifa hilo mara nyingi hawapati fursa za haki au za kisheria.

Msumbiji ni moja ya nchi tatu za Kusini mwa Afrika kuridhia mkataba huo wa wahamiaji na familia zao.