Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata upasuaji mmoja wa fistula Niger ni ushindi- Dkt. Idrissa

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J.Mohammed(katikati) akiwa amesimama na Margot Wallstrom, waziri wa mabo y njewa Sweden(k) na Dkt Lalla Issoufou Mohamadou,mke wa rais(kulia) katika kituo cha kitaifa cha kutibu fistula Niamey, Niger.
UNFPA/Ollivier Girard

Afya

Vituo vya kutibu wagonjwa wa Fistula nchini Niger ni kimbilio kwa wasichana wanaopata tatizo hilo baada ya kuchanika pindi wanapojifungua kutokana na kuozwa wakiwa na umri mdogo.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J.Muhammed amesema hayo  baada ya kutembelea kituo cha kitaifa cha kutibu fistula na kukutana na wagonjwa pamoja na madaktari wao huko Niamey mji mkuu wa Niger.

Naibu Katibu ambaye ameongoza ujumbe wa pamoja wa Umoja wa mataifa na Muungano wa Afrika, amesema unyanyapaa wanaoupata wanawake na wasichana wanaougua fistula sio tu wa kimwili na kifikra bali pia ndani ya jamii yao na baada ya kukataliwa hujikuta hawana pa kwenda.

Fistula ni tatizo la kiafya linalotokana na kuwepo kwa tundu kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke au hata na njia ya kubwa na husababishwa na uzazi pingamizi.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed azuru kituo cha kitaifa cha Nasuri(Fistula) Niamey, Niger, akiwa na Margot Wallstrome, waziei wa mambo ya nje wa Sweden na Dkt Lalla Malika Issoufou Mohamadou,mke wa rais (kulia).
UN/Ollivier Girard

Miongoni mwa wanufaika wa kituo hicho ni Kodi Moumdau mwenye umri wa miaka 23 ambaye sasa anajiona ana bahati ya mtende kwa kuwa ametibiwa fistula na kupona.

Kodi alizaa mtoto mfu na katika mchakato huo alichanika na kupata fistula hali iliyomsababishia kushindwa kuzuia haja na hivyo kumletea fedheha.

Katika kituo hicho cha kitaifa cha kutibu fistula, moja ya vituo vipya 11 nchini Niger vya kutibu ugonjwa huo, kuna wanawake 69 ambao kati yao 42 wanasubiri kufanyiwa upasuaji ili kutibu fistula.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Dkt Abdoulaye Idrissa amesema hufanya operesheni sita akisema kuwa hata upasuaji mmoja ni ushindi.

Hata upasuaji wa mmoja ni ushindi

Amesema kuwa wana kazi ngumu kwani idadi ya wahitaji ni kubwa na hivyo kila mwaka wanaongeza idadi ya mabingwa wa upasuaji, na wanafungua zahanati mpya ili waweze kufika katika sehemu zote nchini Niger.

Ametaja sababu ya ongezeko la visa vya fistula kuwa ni umaskini,kutojua kusoma wala kuandika kutopata huduma za kiafya pamoja na suala la kijamii kama vile  ndoa za utotoni.

Dkt. Idrissa amesema wastani wa umri wa  wagonjwa anaotibu ni miaka 18, lakini kila mara hushuhudiawatoto wa kike wenye umri mdogo kama vile 12 au 13 na kuongeza kuwa nafasi kwa  watoto wadogo kuweza kupata fistula ni kubwa kwani mwili wao huwa bado haujakomaa kuweza kujifungua salama.