Sitisheni mapigano Syria ili misaada ifikie wahitaji- Grandi.
Nina wasiwasi na mapigano Kusini Magharibi mwa Syria ambapo raia wa kawaida ndio wamenaswa katika mapigano hayo.
Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi amesema hayo leo kupitia taarifa iliyiotolewa mjini Geneva Uswisi.
Mapigano hayo yanahusisha mashambulio ya anga na makombora mazito ambapo watu takriban watu 750,000 wako hatarini huku wengine 320,000 hawana makazi wakiishi kwenye mazingira magumu.
Kati yao yao 60,000 wamepiga kambi huko Nasib/Jaber ambacho ni kituo cha kuvuka mpaka kuingia Jordan.
“Ingawa jamii za Syria zimewakaribisha watu hao waliopoteza makazi yao, bado wengiwanalazimika kulala nje ama wengine katika vibanda vya muda tu ambavyo si salama. Miongoni mwao ni watoto, wanawake, wazee, majeruhi na wagonjwa,” amesema Bwana Grandi.
Ameongeza kuwa miongoni mwa waliopoteza makazi ni wafanyakazi wa kutoa misaada ambao walijitolea kwa dhati kusaidia raia wakati wa mgogoro.
Kamishna Mkuu huyo wa wakimbizi amesema kuwa kipaumbele sasa ni kutafuta suluhisho la kisiasa ili kuweza kuwaondolea mateso zaidi watu wa Syria.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanajaribu kadri ya uwezo wao kutoa msaada muhimu kwa wakazi wa kusini-magharibi mwa Syria na pia katika upande mwingine Jordan.
Hata hivyo hali ya kiusalama inadumaza juhudi za kuwafikia watu hao.
Bw Grandi ameziomba pande zote kuzidisha juhudi za kukomesha makabiliano, waruhusu misaada muhimu ifikishwe kwa walengwa na pia wakubali watoa misaada ya kibinadamu kufanya kazi yao ya kuhamisha majeruhi na pia kuwapatia wahitaji makazi ya muda.
Ameongeza kuwa ulinzi na usalama wa raia na watoa msaada ni muhimu mno.