Viongozi Sudan Kusini pigeni moyo konde- UN
Hatutachoka kutafuta amani ya kudumu katika taifa la Sudan Kusini, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J.Mohammed wakati wa ziara yake aliyoanza leo nchini humo yenye lengo la kukuza umuhimu wa wanawake katika kuzuia migogoro.
Amesema ni kwa muktadha huo amekwenda nchini humo ambapo pia lengo ni
(Amina J. Mohammed)
“Kuwaambia nilichosikia viongozi wa Afrika wakisema, ni kuwa sasa viongozi nchini Sudan Kusini sharti wapige moyo konde na wabadilike pamoja na kuwajibika kuhusu amani ya nchi yao.”
Kuhusu unyanyasaji wa kingono katika migogoro, Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa Umoja wa Mataifa unajaribu kadri ya uwezo wake kulishughulikia suala hilo.
(Amina J. Mohammed)
“ Hapa tuna mshauri maalum wa dhuluma za kingono dhidi ya wanawake katika sehemu za migogoro ya kivita ili kuweza kuwasilisha malalamiko yenu kwa jamii ya kimataifa na hivyo tuwezeshe viongozi kufanya mambo mazuri.”
Katika ziara hiyo, Bi. Mohammed anaandamana na mjumbe maalum wa Muungano wa Afrika anayehusika na masuala ya wanawake, amani na usalama Bineta Diop.
Akiwa nchini humo Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anakutana na makundi mbalimbali pamoja na ya viongozi wa wanawake, kidini na wa makundi ya kiraia.