Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la idadi ya maafa pwani ya Libya inasikitisha

Wakimbizi wanaovuswa baharini Mediterranea kuelekea Ulaya. Picha: UNHCR/A. D'Amato

Ongezeko la idadi ya maafa pwani ya Libya inasikitisha

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya wahamiaji 200 wamekufa maji kwenye baharí ya Mediterranea katika kipindi cha siku tatu zilizopita na kufanya idadi ya vifo mwaka huu kufikia takriban elfu moja, hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji duniani, IOM.

Zahma hiyo ilianza Ijumaa wakati watu takriban 103 wakiwemo watoto watatu walipokufa maji baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya Libya.

Walinzi wa pwani ya Libya waliokoa watu 16 ambao ni wanaume kutoka Gambia, Sudan, Yemen, Niger na Guinea.

Tukio hilo lilifuatiwa na ajali nyingine ambapo boti nyingine ndogo ilizama pembeni mwa mji wa bandari wa Al Khums, mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Chombo hicho kilikuwa kimebeba watu wengi ambapo 41 walinusurika kifo huku watu 100 wakiripotiwa kupotea.

Wakati huo huo walinzi wa pwani ya Libya walizuia boti ndogo zilizokuwa zikielekea baharini na kurejesha takriban wahamiaji elfu moja katika pwani.

Kwa mujibu wa taarifa ya IOM, watu hao ambao wanashikiliwa katika vituo ambako wanapokea msaada walipewa chakula, maji na huduma ya afya pamoja na huduma ya dharura.

Mwaka huu walinzi wa pwani ya Libya wamerejesha takriban watu elfu kumi katika maeneo salama, kwa mujibu wa mkuu wa ujumbe wa IOM , Othman Belbeisi,  Libya akitaja kuongezeka kwa maafa kwa kiwango kinachotia wasiwasi.

Bwana Belbeisi amesema wasafirishaji haramu wanalaghai wahamiaji kuondoka kabla ya msako unaofanywa na Ulaya.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, William Lacy Swing atasafiri kuelekea Tripoli wiki hii kushuhudia hali ya wahamiaji waliookolewa na waliorejeshwa pwani.

IOM imesema imejizatiti kuhakikisha haki za binadamu za wahamiaji wote zinaheshimiwa wakati juhudi zikielekezwa kukomesha biashara ya usafirishaji haramu wa watu.