Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yamteua Ben Stiller kama balozi wake mwema

Balozi mwema wa UNHCR Ben Stiller azuru wakimbizi Guaemala
UNHCR/Michael Muller
Balozi mwema wa UNHCR Ben Stiller azuru wakimbizi Guaemala

UNHCR yamteua Ben Stiller kama balozi wake mwema

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limemtangaza mcheza filamu na mtayarishaji wa filamu Ben Stiller kuwa balozi wake mwema.

UNHCR imetoa tangazo hilo wakati huu ambapo Bwana Stiller amemaliza ziara yake na shirika hilo huko Guatemala ambako alikutana na baadhi ya wanaume, wanawake na watoto kutoka maeneo ya kaskazini mwa Amerika ya Kati ambao wamelazimika kukimbia makwao kufuatia vurugu.

Akizungumzia uteuzi huo mcheza filamu Stiller amesema amepokea taarifa hizo kwa unyenyekevu na kwamba anajivunia kuchukua nafasi hiyo ya balozi mwemwa wa UNHCR, akiongeza kuwa shirika hilo linafanya kazi kote ulimwenguni likisaidia wanaume, wanawake na watoto ambao wanakimbia vita, ukatili na mateso.

Bwana Stiller amesema akiwa Guatemala ameshuhudia watoto na familia waliokabiliwa na ukatili usioelezeka na kwamba wanahitaji msaada na UNHCR na wadau wake wako mashinani kutoa msaada wanaohitaji..

Aidha ameongeza kuwa kama balozi mwema atafanya kila awezalo kwa ajili ya kupaza sauti za wakimbizi na kuwahimiza wengine kuungana naye kwa ajili ya wakimbizi milioni 68 kote ulimwenguni.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amesema Stiller atakuwa balozi mwema mzuri kwani ameshuhudia nia yake na uwezo wake wa kuzungumzia suala la uhamiaji kwa njia yenye ari na inayoshawishi.

Bwana Stiller amekuwa akishirikiana na UNHCR  tangu mwaka 2016, akikutana na wakimbizi walioko Ujerumani na Jordan. 

Mcheza filamu huyo ambaye anajulikana kwa uigizaji katika filamu kama Dodgeball, Zoolander na Meet the Parents ameshiriki katika miradi ya UNHCR ikiwemo kampeni ya #withrefugees.

Kadhalika hivi majuzi katika maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani Juni 20 alifanya filamu na mkimbizi kutoka Iraq ya kupika chakula cha kitamaduni kutoka nyumbani Iraq na kumletea mawazo ya utoto wake akiwa Baghdad kabla ya kulazimika kukimbia.