Vikosi vya kimataifa vyashambuliwa nchini Mali, UN yalaani

1 Julai 2018

Siku mbili tu baada ya shambulio huko nchini Mali, hii leo shambulio lingine limetokea na sasa ni dhidi ya vikosi vya kimataifa.

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la leo huko Gao, kaskazini mwa Mali dhidi ya vikosi vya kimataifa, shambulio ambalo limesababisha vifo vya raia wawili na watu wengine 15 wamejeruhiwa.

Miongoni mwa majeruhi ni watendaji wa operesheni ya jeshi la Ufaransa nchini Mali, iitwayo Barkhane, ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres pamoja na kulaani ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Mali.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnkuu Katibu Mkuu pia akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi huku akisisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kusaidia juhudi za Mali na wananchi wake za kuleta utulivu nchini mwao.

Amesema watafanya hivyo kwa kushirikiana na vikosi hivyo ya kimataifa vinavyofanya kazi kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la umoja huo.
 
Shambulio hili la leo linafuatia shambulio lingine la Ijumaa huko Mopti lililofanywa dhidi ya kikosi cha kundi la nchi tano za ukanda wa Sahel, G5 ambazo zinasaidia kuimarisha usalama nchini Mali.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud