Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani shambulio dhidi ya makao makuu ya G5, Mali

Dakitari wa MINUSMA akitoa huduma ya kwanza kwa majehuri wa shambulio lakigaidi.
MINUSMA
Dakitari wa MINUSMA akitoa huduma ya kwanza kwa majehuri wa shambulio lakigaidi.

UN yalaani shambulio dhidi ya makao makuu ya G5, Mali

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio dhidi ya makao makuu ya kikosi cha pamoja cha nchi 5 za ukanda wa Sahel, G5 huko Mopti nchini Mali.

Yaelezwa kuwa watu kadhaa waliuawa pindi shambulio hilo lilipofanyika siku ya Ijumaa kwenye jengo lao la Sévaré, aikiwemo askari wa G5 na wanajeshi wa Mali.

Kikosi hicho kinajumisha wanajeshi kutoka Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu amerejelea umuhimu wa kikosi hicho katika kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali kwenye ukanda wa Sahel.

Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa iongeze usaidizi wake kwa kikosi hicho cha pamoja.

Halikadhalika amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA unaendelea kupatika G5 msaada wa vifaa kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la umoja huo.

Bwana Guterres ametumia pia fursa hiyo kutuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulio hilo huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa kulaani shambulio hilo likisisitiza umuhimu wa kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa tukio hilo.

Wajumbe wa baraza hilo wamekaribisha azma ya nchi hizo zinazounda kundi la G5 ya kuendelea kushikamana kukabiliana na uagidi na misimamo mikali kwenye ukanda huo wa Sahel ikiwemo kupitia uimarishaji wa jeshi hilo la pamoja.

Wamesema wataendelea kufuatilia kinachoendelea kwenye ukanda huo sambamba na kusaidia kikosi hicho cha pamoja.