Mpango wa kusaidia Sahel wazinduliwa leo, utajiri wa ukanda huo wawekwa bayana

Umoja wa Mataifa umesema rasilimali lukuki zilizopo kwenye ukanda wa Sahel ni moja ya suluhu mujarabu ya matatizo yanayokabili eneo hilo.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi, Mohammed Ibn Chambas amesema hayo leo huko Nouakchott, Mauritania wakati wa uzinduzi wa mpango wa usaidizi na ujumuishi kwa nchi za Sahel.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed, Bwana Chambas amewaeleza washiriki wa kikao cha ngazo ya juu kuwa, “mara nyingi simulizi kuhusu Sahel hupuuzia maliasili lukuki, utajiri wa utamaduni na rasilimali watu. Sahel imebarikiwa na rasilimali watu, maliasili na tamaduni. Eneo hili lina uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati rejelevu. Bila kusahau madini na uvuvi,” amesema Bwana Chambas.
Hata hivyo amesema utajiri huu utakuwa na maana iwapo watashughulikia mzizi wa janga la sasa huko Sahel.
Ni kwa mantiki hiyo amesema mpango wa usaidizi kwa Sahel ambao jana umeungwa mkono na nchi zote 10 za ukanda huo ndio mwelekeo sahihi wa kuleta ustawi kwenye eneo hilo.
“Mpango huu ni wenu. Umeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya watu na nchi hizi bila kusahau wadau wa kikanda.
Nchi hizo 10 za ukanda wa Sahel ni Mauritania, Mali, Niger, Cameroon, Chad, Senegal, Gambia, Guinea, Burkina Faso na Nigeria.
Nchi za ukanda wa Sahel ni Mauritania, Mali, Niger, Chad, Cameroon, Senegal, Gambia, Guinea, Burkina Faso na Nigeria.
Mpango huo una maeneo sita ambayo ni ushirikiano mpakani, kulinda na kuendeleza amani, ukuaji uchumi na kupata huduma za kijamii, mabadiliko ya tabianchi, mnepo na uhakika wa chakula, uwezeshaji wanawake na vijana pamoja na kupata nishati rejelevu.
Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu amesema zaidi ya yote mpango huo wa usaidizi utasaidia uratibu wa harakati za kunasua ukanda wa Sahel.
Hata hivyo amesihi kuwa wanawake na vijana washirikishwe.
“Sisi tumeazimia kufanya kazi na ninyi nyote na wadau wengine wote ambao mipango yao inaendana na mkakti huu. Na tufanyavyo hivyo, wanawake na vijana pamoja na fursa za ajira ni masuala mtambuka. Tunahitaji kuweka fursa za vijana wa kike na wa kiume ili kuwaepusha na safari za hatari za uhamiaji,” amesema Bwana Chambas .
Ameisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa kwa upande wake unaamini kuwa wakati ni huu wa kuhamasisha uwekezajj wa umma na binafsi na pia kujenga uchumi thabiti, kuwezesha wananchi na kufurahia utu na amani.