Acheni kuwaweka rehani raia wa Syria - Zeid

29 Juni 2018

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameonya juu ya janga linaloendelea huko jimbo la Daraa nchini Syria wakati huu ambapo ghasia zinazidi kuongezeka.

Katika taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi, Bwana Zeid ametoa wito kwa pande zote kwenye mzozo huo kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa sharia za kimataifa na kuepusha kurejea kwa umwagaji damu na machungu yaliyoshuhudiwa mapema mwaka huu huko Ghouta mashariki.
 
“Nchini Syria watu wanageuzwa rehani na makundi mbalimbali. Nawakumbusha  wote wanaohusika katika mgogoro huo kuwa  sheria za kimataifa zinamtaka kila mmoja  kufanya kila awezalo kuwalinda raia na pia naomba muwape njia salama ya kupitia waondoke kwa wale wanaotaka ilhali wale wanaoamua kubaki wabaki salama wakilindwa,” amesema Kamishna Zeid
 
Bwana Zeid amesema hadi sasa maelfu ya watu wameripotiwa kuyahama makazi yao na kukimbilia maeneo ya magharibi mwa Daraa ikiwemo Nawa na Jaseem na pia kwenye mpaka wa Syria na Jordan.
 
Amesema wengi wao wamekwama jangwani bila huduma kama vile chakula na maji wakati huu ambapo tarehe 26 mwezi huu, Jordan ilitangaza kuwa mpaka wake na Syria utaendelea kufungwa.
 
Zaidi ya hayo amesema pia kuna hatari kuwa vita vikipamba moto raia wengi watajikuta wamebanwa katikati ya majeshi ya serikali ya Syria na washirika wake kwa upande mmoja, na makundi ya upinzani na wanamgambo wa ISIL kwa upande mwingine.
 
Halikadhalika amezungumzia ripoti ambazo wamepokea kuwa siku chache zilizopita raia walidaiwa malipo kidogo walipokuwa wanapita vizuizi vinavyodhibitiwa na majeshi ya  serikali huko maeneo ya kusini- mashariki na maeneo ya magharibi mwa Daraa.
 
Tayari vikosi  vya serikali na washirika wake  vimeteka  mji muhimu wa Busr Al-Harir pamoja na miji mingine mashariki mwa Daara katika eneo la Lajat.
 
Kama hiyo haitoshi, “wapiganaji wa ISIL, wanaodhibiti eneo la Yarmouk magharibi mwa Daraa hawakubalii raia wa kawaida kuondoaka kutoka maeneo wanayodhibiti,” amesema Kamishna Zeid.
 
Jimbo la Daraa lipo kwenye maungano ya kuelekea Jordan, katika milima ya Golan ambayo inakaliwa kwa nguvu na Lebanon.
 
Mwezi julai ya mwaka jana eneo hilo lilitangazwa kama eneo lisilokuwa na migogoro katika makubaliano ya pande tatu ya kusitisha vita ambapo Marekani, Urusi na Jordan zilitajwa kuwa wadhamini.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud