Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji idadi kubwa zaidi ya wabunge wanawake- Guterres

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa wabunge wa kimataifa katika makao makuu
IPU
Baadhi ya wabunge wa Umoja wa wabunge wa kimataifa katika makao makuu

Tunahitaji idadi kubwa zaidi ya wabunge wanawake- Guterres

Masuala ya UM

Kwa mara ya kwanza, Umoja wa Mataifa unaadhimhisha hii leo siku ya mabunge duniani, ikiwa ni siku pia ambayo Umoja wa Mabunge duniani, IPU ulianzishwa mwaka 1889.

Katika ujumbe wake kwa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua ya kutenga siku hii ni kwa kuzingatia dhima ya msingi ambayo inatekelezwa na mabunge kote duniani.

Amesema yeye binafsi akiwa mbunge mstaafu, alishuhudia wajibu wa kuwawakilisha wananchi na kujaribu kusongesha matarajio yao.

“Mabunge ni msingi wa demokrasia, ni muhimu kwa watetezi wa haki za binadamu na pia inaunganisha masuala ya kitaifa na kimataifa,” amesema Katibu Mkuu Guterres akitanabaisha kuwa kupitia sheria na kupitisha maamuzi, mabunge yanaweza kuchangia ipasavyo katika malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 
Amesema SDGs ndio mpango wa Umoja wa Mataifa wenye malengo ya kuhakikisha dunia ina ustawi, ina mnepo na zaidi ya yote inashamiri. 
Hata hivyo amesema bado mabunge  yamesheheni idadi kubwa zaidi ya wanaume, akisema dunia inahitaji idadi kubwa zaidi ya wabunge wanawake.

Kwa mantiki amesema katika siku hii ya mabunge anaahidi kushikamana na wabunge kote duniani wakati huu wanapohaha kuhudumia wananchi wao.

 

Nao Umoja wa Mabunge duniani, IPU katika wavuti wake umechapisha taarifa inayohoji ustawi wa mabunge duniani hivi sasa, wakati huu ambapo wabunge wanakabiliwa na vitisho pamoja na idadi ya wabunge wanawake inasuasua.

IPU inasema ingawa kumekuwepo na nuru kutokana na idadi ya wanawake wabunge kuongezeka kwingineko bado katika nchi zingine idadi hiyo ni finyu.

Takwimu za IPU zinaonyesha kuwa Rwanda ndio inaongoza duniani kwa kuwa na asilimia 61.3  ya wabunge wanawake kati ya wabunge 80 ikifuatiwa na Cuba.