Warohingya uso kwa uso na Guterres huko Cox’s Bazar

Wakimbizi takribani milioni moja wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar ambao sasa wamekimbilia Bangladesh kutokana na mateso huko nyumbani , jumapili hii watapa ugeni wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Wakati wa ziara hiyo akiambatana na Rais wa Benki ya Dunia, Katibu Mkuu atashuhudia hali halisi ya madhila wanayokumbana nayo wakimbizi hao ambao wengi wao walianza kumiminika kwenye eneo hilo baada ya mapigano kushamiri jimboni Rakhine nchini Myanmar mwezi Agosti mwaka jana.
Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, ziara hiyo itaangazia pia ukarimu wa Bangladesh wa kuhifadhi wakimbizi hao na pia umuhimu wa jamii ya kimataifa kuchukua hatua zaidi.
Wakati wa ziara hiyo Bwana Guterres na Bwana Jim watakuwa na mazungumzo na maafisa waandamizi wa Bangladesh akiwemo Waziri Mkuu Sheikh Hasina kwenye mji mkuu Dhaka.
Siku ya Jumatatu, watasafiri kuelekea eneo la Cox’s Bazar ambako watakuwa na mazungumzo na wakimbizi warohingya, wafanyakazi wa misaada na wachehemuzi wa ufadhili kutoka kwa wahisani.
BENKI YA DUNIA YATANGAZA DOLA MILIONI 500 KUNUSURU WAROHINGYA
Siku ya Alhamisi wiki hii, Benki ya Dunia ilitangaza mkopo wenye masharti nafuu wa dola milioni 500 wa kusaidia Bangladesh kushughulikia mahitaji ya warohignya.
Fedha hizo ni kwa ajili ya masuala ya elimu, afya, maji, udhibiti wa majanga na ulinzi wa kijamii.
Rais wa Benki ya Dunia amesema mkopo huo nafuu utasaidia nchi hiyo kunusuru wakimbizi wakati huu wa uhitaji.
“Tumeguswa sana na machungu ya warohingya na tuko tayari kusaidia hadi pale watakaporejea nyubmani kwa usalama, bila shinikizo na katika hali ya kiutu. Na wakati huohuo tunaendelea pia kusaidia Bangladesh na jamii za wenyeji zinazohifadhi wakimbizi, ambao wameonyesha ukarimu mkubwa kwa kuwakaribisha wakimbizi,” amesema Bwana Jim, Rais wa Benki ya Dunia.
Bwana Guterres ataambatana pia na maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa wakiwemo Kamishna Mkuu wa wakimbizi, Filippo Grandi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la idadi ya watu la umoja huo, UNFPA, Natalia Kanem.
“Watatathmini hali ilivyo kwa wakimbizi wapya warohingya wanaowasili Bangladesh na pia kuangalia maendeleo ya mchakato wa kuhakikisha wanareja nyumbani kwa hiyari, utu na kwa usalama kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa,” amesema Bwana Dujarric.
Kabla hata ya kuanza kumiminika kwa warohingya mwezi Agosti mwaka jana, tayari wakimbizi wengine 200,000 walikuwepo Bangladesh kutokana na mateso wanayopata nchini mwao Myanmar.
Ijapokuwa idadi ya wanaowasili imepungua na makubaliano yamefikiwa ya kuwezesha warejee nyumbani, bado mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema mazingira si shwari kwa wakimbizi hao kuweza kurejea nyumbani.
Harakati hizo zikiendelea, nayo mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yanaendelea na kazi ya kuhakikisha mvua za monsuni hazileti madhara ya mafuriko na vifo kwa wakimbii hao huko Cox’s Bazar.
Hadi tarehe 24 mwezi uliopita takribni wakimbizi 905,00 warohingya walikuwa wamesaka hifadhi Cox’s Bazar.
Ili kusaidia mahitaji yao yanayoongezeka kila uchao, Umoja wa Mataifa ulitangaza ombi la pamoja mwezi Machi mwaka huu la dola milioni 951 kwa ajili ya wakimbizi na jamii za wenyeji. Hata hivyo hadi sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimia 18 pekee