Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 100 wafa maji Mediteranea

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea

Watu 100 wafa maji Mediteranea

Wahamiaji na Wakimbizi

Bahari ya Mediteranea yazidi 'kumeza' watu, manusura wasimulia walivyopata kiwewe.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesikitishwa na janga la hivi karibuni zaidi la watu wapatao 100 kuzama na kufa maji kwenye bahari ya Mediteranea.

Taarifa ya UNHCR imesema katika tukio hilo la leo watu  hao wamekufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya Tajoura nchini Libya ambapo watu wengine 23 wamenusurika.

Kwa mujibu wa manusura, boti hilo la mpira ambalo halipaswi kabisa kusafirisha abiria, lilikuwa limejaa kupita kiasi na kwamba manusura hao walilazimika kuogelea kwa saa moja kabla ya kuokolewa na walinzi wa pwani ya Libya.

 “Hii ni siku ngumu zaidi katika maisha yangu. Sikufahamu iwapo nijiokoe mimi mwenyewe, wanangu au marafiki zangu,” amesema mmoja wa manusura baada ya kuokolewa.

Miongoni mwa waliofariki dunia ni wanaume 70 na wanawake 30 na watoto wachanga watatu. 

Yaelezwa kuwa maiti 16 wameopolewa ilhali maiti wengine 80 bado wako baharini.

UNHCR imesema ina hofu kubwa juu ya ongezeko la watu wanaokufa maji wanaposafiri kupitia njia ya kati mwa Mediteranea na hivyo inatoa wito kwa juhudi za kimataifa za kuepusha janga zaidi.

Wakati huo huo, inaelezwa kuwa leo Ijumaa pia walinzi wa pwani wa Libya waliwafikisha katika kituo cha wanamaji cha Tripoli  wakimbizi na wahamiaji wapatao 300 ambapo miongoni mwao ni watoto 15 na wanawake 40.

UNHCR na wadau wake walikuwepo kwenye eneo hilo na kuwapatia wakimbizi hao mahitaji ya dharura ikiwemo matibabu na misaada ya kibinadamu kabla ya kuhamishiwa vituo ambako watashikiliwa wakisubiri mchakato wa utambuzi.