Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usitishwaji mapigano Hodeida ni ufunguo wa kuanza mazungumzo kuleta amani Yemen-Griffiths

Mashambulizi ya mara kwa mara nchini Yemen yanaweka raia katika hatari.
Giles Clarke/UN OCHA
Mashambulizi ya mara kwa mara nchini Yemen yanaweka raia katika hatari.

Usitishwaji mapigano Hodeida ni ufunguo wa kuanza mazungumzo kuleta amani Yemen-Griffiths

Amani na Usalama

Nchini Yemen kuna nuru sasa ya mazungumzo kati ya pande kinzani. Umoja wa Mataifa umeelezea matumaini hayo wakati huu ambapo tayari chombo hicho kimeruhusiwa kusimamia bandari muhmu ya Hodeidah.

Matukio kwenye uwanja wa vita ni kikwazo kwenye mchakato wa amani nchini Yemen, lakini mazungumzo ya kisiasa ni kipaumbele cha juu cha kutatua mgogoro huo, amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen katima mahojiano maalum na Idhaa ya  Umoja wa Mataifa.

Bwana Griffiths amesema kuwa kipaumbele kikuu na cha juu ni kuwezesha mazungumzo ili kukomesha vita akisema kuwa “Hodeida ni suala la kipekee na muhimu, lakini si muhimu zaidi kuliko suala la suluhisho la kisiasa." 

Akisisitiza kwamba kuzuia shambulio la Hodeida ni mojawapo ya vipaumbele vya juu, bBana Griffiths amesema kuwa ni wazi kutokana na majadiliano na pande zote kwenye mzozo kuwa suluhisho la mgogoro wa Hodeida linategemea kuanzishwa upya kwa mazungumzo ya kisiasa. 

Matukio kwenye uwanja wa vita ni kikwazo kwenye mchakato wa amani nchini Yemen

Mashambulizi ya mara kwa mara nchini Yemen yanaweka raia katika hatari.
Giles Clarke/UN OCHA
Mashambulizi ya mara kwa mara nchini Yemen yanaweka raia katika hatari.

Akielezea hatua zilizopigwa kuelekea kufanikisha mazungumzo, ametaja mafanikio akisema kwanza ni….

“Kwamba hakujakuwa na mashambulizi yoyote dhidi ya mji au bandari ya Hodeida  ni kutokana na mazungumzo ambayo tumefanya na pande husika. Kumekuwa na mapigano vitongoji vya uwanja wa ndege lakini hakuna uhasama wa kuripotiwa katika bandari. Kitu cha pili cha kujivunia ni kwamba  uongozi wa Ansar Allah umetupatia sisi Umoja wa Mataifa fursa ya kusimamia bandari ya Hodeida  kwa kutegemea kusitisha mapigano,  na tatu ni kwamba tunaendelea kutathmini ni nini kinapaswa kukubaliwa ili kuzuia mapigano na mashambulizi yoyote dhidi ya Hodeida.”

Kuhusu wakati ambao majadiliano yatafanyika, Griffiths amesema angependa kupata pande husika  katika wiki chache zijazo, huku akiongeza kuwa kuanza upya kwa mazungumzo kumechukua  muda mrefu na watu wa Yemeni wanatarajia yafanyike haraka iwezekanavyo.

Nchini Yemen kusambaratika kwa miundombinu ya afya na ile ya  majisafi na majitaka kumesababisha kazi ya kukabili magonjwa kuwa ya shida.
UNICEF/UN065871/Alzekri
Nchini Yemen kusambaratika kwa miundombinu ya afya na ile ya majisafi na majitaka kumesababisha kazi ya kukabili magonjwa kuwa ya shida.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa kama kipaumbele kwa watu wa Yemen ambao wote wanalilia amani.Bwana Griffiths amesema anatarajia kuelezea Baraza la Usalama masuala muhimu ya kufanikisha majadiliano na kujadili nafasi ya Umoja wa Mataifa katika majadiliano hayo.

Aidha ametaja changamoto kubwa kutatua mzozo wa Hodeidah ni

“Changamoto kubwa ni vita, najua hilo ni kama kitu cha kawaida kusema lakini kizuizi kikubwa dhidi ya mchakato wa kuleta amani ni matukio ya uwanja wa mapigano na ni moja ya sababu mbili ya sisi kukataa mashambulizi dhidi ya Hodeidah. Nyingine ni athari za kibinadamu  kufuatia mashambulizi  na kama nilivyoelezea Baraza la Usalama mwezi Aprili, ni vita ndivyo vitatuzuia kuleta pande husika katika meza ya majadiliano  na hiyo ndio maana tunatolea wito pande husika kusitisha mapigano kama sehemu ya majadiliano.”