Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu yakaribisha uamuzi wa kesi dhidi ya Noura

Picha:MONUSCO
Ubakaji na ukatili wa kingono ni ukiukaji wa haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu yakaribisha uamuzi wa kesi dhidi ya Noura

Haki za binadamu

Hatimaye Sudan yapunguza adhabu dhidi ya mwanamke aliyemuua mumewe ambaye alikuwa akimbaka mara kwa mara.

Tunakaribisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa huko Khartoum, Sudan wa kufutilia mbali hukumu ya kifo dhidi ya Noura Hussein. 

Kauli hiyo imetolewa leo na ofisi ya haki za binadamu mjini Geneva Uswisi kufuatia uamuzi huo wa Jumanne.

Bi.Hussein alikuwa amehukumiwa kifo mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya kumchoma kisu na kumuua mumewe ambaye alilazimishwa kuolewa naye na ambaye alishtaki kumbaka mara kwa mara.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu  Ravina Shamdasan, amesema licha ya kwamba hawana maelezo kamili ya uamuzi katika hatua hii, taarifa walizo nazo ni kwamba hukumu ya kifo imebadilishwa kuwa kifungo cha jela cha miaka mitano.

Msemaji huyo ameongeza kuwa katika wito wao mwezi uliopita kwa serikali ya Sudan waliwahimiza kuchukua fursa hii kutuma ujumbe wa wazi kwamba unyanyasaji wa kijinsia hauwezi kuvumiliwa nchini humo, na kuweka sheria  kuwa ubakaji ndani ya ndoa kuwa uhalifu.

Ofisi ya haki za bindamu imeelezea utayari wake kufanya kazi na serikali ya Sudan kwa kuweka sheria zake kulingana na viwango vya haki za binadamu, huku ikiahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka ya Sudan katika hilo.