Gari la kwanza baada ya miaka 20 laleta msisimko katika utoaij chanjo DRC

29 Juni 2018

Ufikishaji wa chanjo dhidi ya Ebola kwenye kijiji cha Bosolo kilichopo jimbo la Equateur nchini Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Congo, DRC umekuwa ni fursa kwa watoto wa eneo hilo kushuhudia gari kwa mara ya kwanza.

Kijiji hicho cha Bosolo kipo takribani kilometa 25 kutoka kituo cha afya cha Iboko jimboni humo, lakini kutokana na ubovu wa barabara, hulazimu gari kutumia saa mbili au zaidi.

Dkt. Ismaila Sani kutoka shirika la afya ulimwenguni ambaye aliongoza msafara huo ukiwa na chanjo, anasema kabla ya wao kwenda, ililazimu kutuma timu ya awali ambayo ilisafiri kwa bodaboda ili kubaini iwapo barabara inapitika au la kutokana na barabara hiyo kuwa nyembamba na miti kusheheni njiani.

Kwa msaada wa wakazi wa eneo hilo, waliweza kufanya marekebisho na walivuka takribani madaraja manne ambayo walikuwa wakipachika magogo ili kuweza kupita.

Dkt. Sani ambaye ni mratibu wa utoaji wa chanjo ya Ebola DRC, anasema hatimaye walifika wakiwa na mahema, vifaa vya matibabu, meza na viti.

WHO
Timu ya WHO kwa msaada wa wakazi wa kijiji cha Bisolo, wakiweka magogo ili gari liweze kuvuka daraja na kuingia kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 25 kutoka kituo cha afya cya Iboko.

Mapokezi yalivuta hisia hususan kwa watoto ambapo mkazi mmoja alitoa shukrani zake kwa kampeni hiyo ambayo imewezesha watoto kuona gari kwa mara ya kwanza.

Kabla ya kuanza kutoa chanjo, wataalamu hao walielimisha wakazi wa kijiji hicho juu ya umuhimu wake na hatimaye waliridhia kupatiwa chanjo hiyo ambapo baada ya kampeni ya siku tatu jumla ya watu 150 waliokuwa wanapaswa kupatiwa chanjo, walikuwa wamepatia chanjo hiyo dhidi ya Ebola.

Katika eneo hilo, WHO ililazimika kufikisha chanjo kutokana na kuthibitishwa kwa kifo cha mtu mmoja dhidi ya Ebola.

Hadi tarehe 20 mwezi huu, takribani watu 3,200 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola kwenye maeneo shukiwa huko jimbo la Equateur pamoja na wahudumu wa afya 13 mjini Kinshasa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud