Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa Myanmar inanizuia nitasaka ukweli wa mateso dhidi ya warohingya- Mtaalamu

Mjumbe maalum wa haki za binadamu kuhusu Myanmar Yanghee Lee
Picha/Jean-Marc Ferré
Mjumbe maalum wa haki za binadamu kuhusu Myanmar Yanghee Lee

Ingawa Myanmar inanizuia nitasaka ukweli wa mateso dhidi ya warohingya- Mtaalamu

Haki za binadamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu  haki za binadamu nchini Myanmar, Yang Lee anatarajia kuanzaziara ya kikazi hapo kesho tarehe 29  kwenye mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka na maeneo mengine ya Cox’s Bazarambako wakimbizi kutoka Myanmar wanaishi katika makazi ya muda.

Hata hivyo mtaalamu huyo kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi anaeleza masikitiko yake makubwa kutokana na uamuzi wa serikali ya Mynmar kuendelea kumzuia kuingia nchini humo kufanya kazi yake licha ya wito kutoka Baraza la Haki za binadamu la kuitaka serikali hiyo ionyeshe ushirikiano.

Amesema licha ya vizuizi vya kikazi ameazimia kuwafikia popote pale walipo wahanga wa vitendo vya ukiukwaji wa haki vilivyofanyika Myanmar ili kusikiliza uzoefu wao na kuelea hali halisi ya haki za binadamu Myanmar.

Katika ziara yake ya siku 9 huko Bangladesh atakutana na maafisa wa mashirika mbalimbali wa Umoja wa Mataifa,viongozi wa serikali, asas za kiraia, wahudumu wa afya katika kambi za wakimbizi mbalimbali ikiwemo nakutembelea kisiwa cha Bashan Char.

Zaidi ya wakimbizi 700,000 wa kabila la rohingya kutoka Myanmar wamekimbilia Bangladesh kuanzia mwezi Agosti mwaka jana kutokana na mashambulizi dhidi yao huko jimboni Rakhine.

Mwishoni mwa ziara yake, Bi. Lee atatoa taarifa ya kile alichoshuhudia na hatimaye kuwasilisha ripoti yake mbele ya mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 23 mwezi Oktoba mwaka huu jijini New York, Marekani.