Watu CAR wanakata tamaa kutokana na hali ya usalama- UN
Watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, wanateseka zaidi kutokana na hali ya usalama kuendelea kuvurugikahuku wakikatishwa tamaa na wale ambao wanapaswa kuwalinda.
Mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa CAR, Marie Thérèse Keita Bocoum amesema hayomjini Bangui, CAR hii leo baada ya kukamilisha ziara ya kikazi ya siku 10 katika nchi hiyo.
Kutokana na aliyoshuhudia, kuharibika kwa hali ya haki za binadamu nchini humo, Bibi Bocoum ameomba kuwepo kwa uratibu mzuri wa juhudi za amani, sheria na kusameheana nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mtaalam huyo amesema, japo serikali inajitahidi kulinda watu wake, bado ina udhibiti mdogo kwenye maeneo yote ya nchi hiyo huku makundi yenye silaha yaliyoko sehemu mbalimbali nchini humo yakiendeleza ukatili.
Ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya kutokuwepo kwa mawasiliano na uwazi baina ya washika dau wanaofanya kazi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati akisema, “nasikitishwa na kuzorota kwa hali ya kibinadamu na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na usalama kufuatia operesheni za kijeshi mwezi Aprili pamoja na matukio ya Bangui mapema mwezi Mei ambapo raia kadhaa walipoteza maisha yao na pia nafasi za kuabudia kushambuliwa.”
Ameomba kuchukuliwa hatua za haraka kuunga mkono huduma za mahakama na pia kurejesha imani ya haki ya ukweli, vyenye lengo la kuzuia kutorudiwa tena kwa migogoro.
Pia Bi. Bocoum, ameshtushwa na ongezeko la visa vya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu pamoja na vifaa vyao na kuwahimiza maafisa wa maeneo hayo kuimarisha utawala wao na pia kulaani vitendo vibaya.
Bi Bocoum atawasilisha rasmi ripoti yake katika Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi tarehe 4 mwezi ujao.