Mapigano kati ya wafugaji na wakulima Afrika yamtia hofu Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ana wasiwasi mkubwa kutokana na matukio ya mara kwa mara ya mapigano kati ya wakulima na wafugaji wanaohamahama kwenye maeneo ya Afrika Magharibi na Kati.
Vyombo vya habari vimetaja moja ya matukio hayo kuwa ni kule nchini Nigeria ambako wakulima na wafugaji hao walipambana mwishoni mwa wiki kwenye jimbo la kati la Plateau na kusababisha vifo vya watu 86.
Mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kupungua kwa ardhi yenye rutuba na malisho ya ng’ombe ni moja ya sababu ya mzozo huo wa ardhi.
Taarifa ya msemaji wake iliyotolewa leo mjini New York, Marekani imesema matukio hayo yanayoambatana na uporaji, ujangili na mauaji ya binadamu yanatishia usalama wa ukanda huo.
Bwana Guterres amelaani vitendo hivyo akisema vinatishia pia kuishi kwa utangamano miongoni mwa jamii za eneo hilo.
Amesisitiza kuwa mashambulizi yoyote yanayolenga raia yanakiuka sheria za kibinadamu za kimataifa.
Amesihi pande zote husika ikiwemo serikali, mashirika ya kikanda, mashirika ya kiraia na wadau wote washirikiane ili kusaka suluhu ya kudumu ya mizozo hiyo ya wafugaji na wakulima.
Katibu Mkuu amesema harakati zozote za kusaka amani lazima zizingatie mifumo ya kikanda pamoja na sharia za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.
Amesisitiza mshikamano kati ya Umoja wa Mataifa na serikali za nchi husika kwenye mzozo huo akisema kuwa yuko tayari kusaidiai juhudi za kikanda na kimataifa katika kusuluhisha mvutano huo kati ya wakulima na wafugaji.