Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dawa mpya kuepusha wanawake na vifo baada ya kujifungua

© UNFPA / Anne Wittenberg
Wauguzi wahudumia kinamama wajawazito katika kituo cha afya cha muda kwenye kambi ya Muna nje ya Maiduguri.

Dawa mpya kuepusha wanawake na vifo baada ya kujifungua

Afya

Katika nchi zinazoendelea, vifo vya wanawake vitokanavyo na kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua linaendelea kuwa mwiba kutokana na changamoto ya uhifadhi wa dawa ya kuzuia tatizo hilo.

Tatizo la wanawake wanaojifungua kutokwa na damu nyingi linaonekana kupata tiba mujarabu baada ya wataalamu kubaini dawa mpya isiyohitaji kuhifadhiwa kwenye jokofu kama ilivyo kwa dawa ya sasa iitwayo Oxytocin.

Dawa hiyo mbadala,  Carbetocin inafuatia utafiti uliofanywa na shirika la afya duniani, WHO na mshirika wake MSD, na majaribio ya dawa hiyo kufanyika katika nchi 10 duniani.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye jarida la kitabibu la New England yakionyesha kuwa Carbetocin haihitaji kuhifadhiwa kwenye jokofu kama ilivyo Oxytocin na hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kutumika kwenye nchi zinazoendelea zilizo na hali ya joto kali.

Halikadhalika dawa hiyo ambayo kitiba ni sawa tu na Oxytocin, inaweza kudumu kwa miaka mitatu ikiwa katika kiwango cha joto cha hadi nyuzi joto 30 katika kipimo cha selsiyasi.

Oxytocin kwa upande wake inahitaji kuhifadhiwa kwenye jokofu kila wakati kwenye joto la nyuzi joto kati ya 2 hadi 8 kwenye kipimo cha selsiyasi.

Gregory Hartl ni mratibu kutoka WHO anaelezea kulikoni walifanya utafiti huo.

(Sauti ya Gregory Hartl)

“Dawa ambazo zimekuwa zinatumika hadi leo hazijaweza kutumika ipasavyo kwa sababu haziwezi kustahimili maeneo yenye joto Kali. Kwa hiyo hii dawa mpya tunaamini inastahimili joto Kali. Kama hivyo ndivyo, na iwapo itaidhinishwa na mamlaka husika, na pia kamati yetu ya mapitio, haya yatakuwa maendeleo makubwa katika kuepusha wanawake na vifo vitokanavyo na kuvuja damu baada ya kujifungua.”

Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka wanawake wapatao 7,000 hufariki dunia kwa kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua, hali inayodokeza kuwa hata watoto wao hufariki dunia ndani ya mwezi mmoja wa kuzaliwa.