Australia yasaidia harakati za UNAIDS huko Asia-Pasifiki

27 Juni 2018

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na UKIMWI -UNAIDS, umekaribisha mchango wa  nyongeza wa zaidi ya dola 977,000 kwa ajili ya harakati zake za kupambana na ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi imesema nyongeza hiyo imetangazwa wakati wa kikao cha bodi ya UNAIDS na zitatumika katika kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi huko Cambodia, Indonesia, Laos na Papua New Guinea.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Michel Sidibe, amesema Australia ni mchechemuzi kiongozi katika harakati dhidi ya Ukimwi katika eneo la  Asia na Pasifiki.

Ameongeza kuwa, "mchango wa ziada ni  ishara muhimu mno wakati huu ili kuhakikisha kila mtu, hususan watu walio hatarini zaidi kupata VVU, wanaweza kujikinga dhidi ya virusi hivyo.”

UNAIDS inasema kuwa pesa hizo zitaongezwa katika fungu la dola milioni 3.3 ambalo Australia iliahidi kuzitoa kwa mpango huo kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mwaka wa 2016 ilikadiriwa kuwa takribani watu milioni 1.5 huko eneo la Asia na Pasifiki wakiwemo watu wazima na watoto walikuwa wanaishi na VVU na watu 260,000 wakiwa ni wagonjwa wapya, huku 170,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.

Karibu nusu ya watu wote wenye VVU kwenye ukanda huo waliweza kupata dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo mwaka wa 2016.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter