Jinamizi la vita nchini Syria halitambui mipaka:UNICEF

27 Juni 2018

Jinamizi la vita na madhila nchini Syria halitambui mipaka, na kwa mara nyingine watoto wamejikuta katikati ya mapigano wasiyojua chanzo chake.

Kauli hiyo imetolewa leo na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta H. Fore, akiweka bayana kwamba machafuko yaliyoshika kasi Kusini Magharibi mwa nchi hiyo yamewatawanya takribani watoto 20, 000 na familia zao katika muda wa siku tatu.

Watoto wanne wameripotiwa kuuwawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ambayo yameharibu vibaya miundombinu ya raia ikiwemo hospital ambayo sasa haiwezi kufanya kazi, hali ambayo Bi. Fore anasema ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Ameongeza kuwa watoto na familia zao wanahitaji chakula, vifaa vya usafi, madawa na ulinzi huku akitoa wito wa wale wanaotaka kukimbia kusaka usalama waruhusiwe kufanya hivyo.

Pia ametoa wito kwa pande kinzani katika mzozo wa Syria kuheshimu misingi ya haki za binadamu na ulinzi wa raia katika vita na kuweka mbele maslahi ya usalama na mustakhbali wa watoto.

UNICEF inasema iko tayari kusaidia walioathirika na machafuko haya mapya na timu zake zimejiandaa kutoa huduma za afya, lishe, maji, vifaa vya usafi, elimu na msaada wa kisaikolojia kwa maelfu ya familia Kusini Magharibi mwa Syria.

Shirika hilo limesisitiza kwamba watoto wa Syria wamepitia madhila mengi yasiyokubalika na hali hiyo asilani haiwezi kuruhusiwa kuwa ada.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter