Mwaka 2017 umekuwa wa dhuluma kubwa kwa watoto:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza makao makuu ya umoja huo, New York
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza makao makuu ya umoja huo, New York

Mwaka 2017 umekuwa wa dhuluma kubwa kwa watoto:Guterres

Amani na Usalama

Mwaka 2017  umekuwa wa kutisha na ulioghubikwa na dhuluma kubwa dhidi ya watoto waishio katika maeneo yenye migogoro, huku idadi ya visa vya ukatili na ukiukwaji wa haki zao vikiongezeka kuliko mwaka uliotangulia.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu athari za migogoro ya silaha kwa watoto, iliyotolewa leo mjini New York Marekani , mwaka  2017 kulikuwa na visa vya ukatili 21,000 ikilinganishwa na 15,500 mwaka 2016.

Ripoti hiyo inamulika kipindi cha kati ya Januari hadi Disemba mwaka 2017 na kuorodhesha aina 20 za ukiukwaji wa haki dhidi ya watoto ikiwemo mauaji, kujeruhiwa, kusajiliwa jeshini na mashambulizi dhidi ya shule pamoja na hospitali.

Ripoti imesema kwa kipindi hicho  visa vya ukiukwaji takriban 6,000 vimetekelezwa na vikosi vya serikali mbalimbali na vingine zaidi ya 15,000 na makundi yenye silaha ambayo  hayana uhusiano na serikali yoyote.

Kwa mujibu wa ripoti kwa visa vya kuwaingiza kwa shuruti  watoto katika makundi ya wapiganaji  zaidi ni 8,000 huku  visa vya mauaji na majeruhi vikifika 10,000 na vya watoto kutekwa vikiongezeka hadi 2,500.

 

Picha hii ya maktaba inaonyesha askari watoto walioachiliwa huru Sudan Kusini
UNICEF/2015/South Sudan/Sebastian Rich
Picha hii ya maktaba inaonyesha askari watoto walioachiliwa huru Sudan Kusini

Ukiukwaji unaoshika nafasi ya nne katika ripoti hiyo ni watoto  kunyimwa msaada wa kibinadamu ambapo visa 1400 vya aina hivyo viliorodhjeshwa na  mashambulizi dhidi ya hospitali na shule yalikuwa zaidi ya 1,100. Na visa vilivyoshika nafasi ya chini ni vya ubakaji na aina nyingine ya unyanyasaji wa kingono visa zaidi ya 900 viliorodheshwa mwaka 2017.

Mabara matatu ndio yaliyomulikwa kwenye ripoti hiyo ambayo ni Afrika, Asia na Amerika ya  Kusini. Kwa upande wa Asia, Afghanistani bado  inaongoza kwa kuwa na visa vingi  vya watoto waliojeruhiwa katika kipindi hicho ambapo 3,179, wavulana kwa wasichana, wameripotiwa ama kuuawa au kujeruhiwa katika kipindi hicho.  Barani Afrika  yametajwa maeneo matatu Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa upande wa kusajili na kuwatumia watoto jeshini ambapo idadi iliongeza maradufu na kufikia watoto 1,049 na Al-Shabab, kundi la wanamgambo wa itikadikali nchini Somalia, liliwachukua mateka watoto 1,600.

Sudan Kusini imetajwa kuwa na visa 783  vya watoto waliokataliwa kupata msaada wa kibinadamu. Nayo makundi ya wapiganaji katika maeneo hayo imeelezwa kuongezeka kutoka 63 ya mwaka 2016 hadi 66 ya mwaka huu. Vikosi sita vya serikali na makundi 57 ya wanamgambo yametajwa kuhusuka na ukatili na ukiukaji wa haki za watoto kwenye mizozo mwaka 2017.