Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudi Arabia waachilieni wanawake mliokamata- Wataalamu

bendera ya Saudi Arabia ikipepea makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York
UN Photo/Loey Felipe
bendera ya Saudi Arabia ikipepea makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York

Saudi Arabia waachilieni wanawake mliokamata- Wataalamu

Haki za binadamu

Wataalam wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa  wameitaka serikali ya Saudi Arabia iwaachilie huru mara moja  wanawake wanaharakati waliowekwa ndani katika msako uliofanyika nchini humo hivi karibuni, wakati huu ambapo taifa hilo limeondoa marufuku ya wanawake kuendesha magari.

 

Katika taarifa yao  ya pamoja, waliyoitoa leo huko mjini Geneva Uswisi, wataalam hao wamesema kuwa tofauti na wakati wa kufurahia ukombozi wa mwanamke wa Saudi Arabia, wanaharakati wanawake wanaotetea haki za binadamu wamekamatwa na kuzuiliwa katika sehemu mbalimbali nchini humo, jambo linalotia hofu na labda ishara  bayana ya jinsi serikali inavyobagua wanawake.

Watalaamu wametaka wanawake hao wote walio kizuizini waachiliwe huru huru mara moja, kwani walikamatwa wakati wanatekeleza wajibu wao  tena kihalali wa kuendeleza na pia kulinda haki za wanawake wa Saudi Arabia .

Halikadhalika wamesema kuwa wanawake wanaotetea haki za wenzao  wanapata shida nyingi nchini Saudi Arabia, sio tu kutokana na kazi yao lakini pia na ubaguzi kutokana na jinsia yao.

Kamatakamata hiyo ilianza tarehe 25 mwezi uliopita ambapo katika kipindi cha wiki tatu, takriban wanaharakati 12 wakiwemo wanawake na wanaume walitiwa mbaroni.

Wengi wao walikuwa wanapigania haki za mwanamke na pia kutaka kuondolewa marufuku dhidi ya wanawake kuendesha magari.

Idadi kubwa ya waliokamatwa  wanakabiliwa na mashtaka makali, jambo ambalo linazusha hofu kuwa kila mmoja huenda akakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20.

Miongoni mwa mashtaka ambayo pengine yanawakabili ni kujihusisha katika mawasiliano na nchi za nje hali inayodaiwa kutishia usalama wa Saudi Arabia na pia kwenda kinyume na maadili ya kidini pamoja na taifa.

Baadhi ya waliokamatwa ni Mohammed Saleh Al-Bajadi, mwanzilishi mwenza wa asasi  ambayo sasa imepigwa marufuku inayotetea haki za raia pamoja na za kisiasa  nchini humo.

Inaripotiwa kuwa Mohammed alitoweka nyumbani kwake tarehe 24 mwezi uliopita. Pia kuna wasiwasi kuhusu mwanamamke mmoja ambaye amezuiliwa na hana mawasiliano na mtu yeyote .

Wataalamu hawa wanasema  wanawasiliana na wakuu wa Saudi Arabia kuhusu suala hilo.