Taarifa za wahamiaji kutelekezwa jangwani zinasikitisha: IOM

26 Juni 2018

Si haki kwa wahamiaji ambao ni pamoja na kina mama wajawazito na watoto kutelekezwa peke yao bila chakula wala maji au kutarajiwa wataweza kutembea kwa miguu maili kadha katika joto kali wakitafuta usalama jangwani.

Kauli hiyo ya masikitiko imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la wahamiaji-IOM, William Lacy Swing, alipogusia taarifa za wahamiaji waliokwama katika eneo la mpaka kati ya Algeria na Niger.

 

Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger
UNHCR/Jehad Nga
Wahamiaji kutoka kituo walimokuwa wakishikiliwa nchini Libya na kusafirishwa hadi Niger

 

Kwa mujibu wa Leonrad Doyle  msemaji wa IOM akiwa  mjini Geneva Usiwisi, IOM inasikitishwa na hatima ya mamia ya wahamiaji ambao hujikuta  wako njia panda  na kuachwa wajitafutie chakula na malazi mpakani mwa Algeria na Niger. Ameongeza kuwa

“Uhamiaji unaodhibitiwa  ndiyo suluhu pekee na wahamiaji wote wanapaswa kutendewa haki na kupewa fursa ya kuishi katika mazingira salama na yenye mpangilio.”

Amesema huo ndio wito wao kwa mataifa yote duniani. IOM inasema idadi ya wahamiaji wanaotembea kwa miguu kupitia jangwa  kutoka Algeria hadi Niger  imeongezeka kwani Mei 2017 wahamiaji 135 walitelekezwa mpakani na sasa imeongezeka hadi 2,888 April mwaka huu.

IOM inakadiria kuwa takriban wahamiaji 11, 276, wanawake na watoto,  walivuka mpaka baina ya nchi hizo mbili mwaka huu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter