Biashara ndogondogo ni gurudumu la SDGs

27 Juni 2018

Umuhimu wa biashara ndogondogo na za wastani, unaelezwa kuwa gurudumu la juhudi  za kusongesha mbele maendeleo endelevu au SDG’s

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa biashara hizo zinafanya kazi nzuri za kimaendeleo kama vile kuinua kiwango cha  ubunifu, uvumbuzi na pia kutoa fursa za ajira katika jamii.

Katika ujumbe wake leo siku ya kimataifa ya biashara ndogondogo na za wastani, Umoja wa Mataifa umesema kwa kutambua mchango wa sekta hiyo katika maendeleo, baraza kuu, lilitenga tarehe 27 Juni ya kila mwaka, kuwa siku ya kimataifa ya  biashara ndogondogo kwa lengo la kuboresha biashara hizo na kuchagiza ufadhili wa kifedha kutoka katika benki mbalimbali na wafadhili wengine na pia kuzihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa  kuhamasisha jamii kuweza kuunga mkono biashara hizo.

 

 Olivia Nankindu mkazi wa Kyotera nchini Uganda.Ni mkulima ambae  amefaidika na mpango wa serikali
Stephan Gladieu/World Bank
Olivia Nankindu mkazi wa Kyotera nchini Uganda.Ni mkulima ambae amefaidika na mpango wa serikali

Biashara hizo zimekuwa tegemeo katika mataifa mengi hususani kwa watu masikini mijini na vijijini. Salome Meto kutoka Kenya ni miongoni mwa wafaidika wa bishahara ndogondogo ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa , alianza na ng’ombe mmoja lakini sasa baada ya mafunzo aliyopata na wakulima wenzie 12000 mambo yamemnyookea ameongeza ng’ombe na mbuzi juu

(SAUTI YA SALOME METO)

“Semina niliyohudhuria  imetusaidia sana kuongeza uzalishaji. Kwa sasa tunatumia chakula kikavu ambacho ni afadhali kwa ngo’mbe wetu kwa sababu tunakitayarisha wenyewe na hudumu kwa muda mrefu.”

Naye Justin Vandevolt, mwenye umri wa miaka 26, sasa ana miliki karakana ndogo yakukarabati kompyuta mjini Cape Town nchini Afrika Kusini kwa ubia na mwajiri wake wa zamani aliyemfanyia kazi kwa muda mrefu

(SAUTI YA JUSTINE VANDEVOLT)

“Kulikuwa na kompyuta nyingi katika karkana yake na kuniuliza ikiwa naweza kuzitengeza nikasema ndio na akanipa kibarua cha kutengeza kompyuta zake.”

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka jana na baraza la kimataifa la biashara ndondogo (ICSB) biashara hizo  na zile za wastani(MSMEs) zinashikilia asilimia 90 ya makampuni yote, huchangia wastani wa  asilimia 60 hadi 70 ya ajira zote na asilimia 50 ya  pato la ndani la mataifa mengi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter