Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya dawa za maumivu bila kibali yasababisha vifo vya watu wengi duniani- UNODC.

Jumba la tiba kwa watumiaji wa mihadarati
UNODC
Jumba la tiba kwa watumiaji wa mihadarati

Matumizi ya dawa za maumivu bila kibali yasababisha vifo vya watu wengi duniani- UNODC.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti ya  mwaka 2018 ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC, imebaini kuwa matumizi ya dawa za  maumivu bila kibali cha madaktari yamesababisha vifo vya zaidi ya asilimia 76 ya watumiaji duniani kote.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo  dawa aina ya Fentanyl inabaki kuwa tatizo kubwa  kaskazini mwa bara la Amerika huku Tramadol ambayo ni dawa ya kupunguza maumivu inabaki kuwa tatizo kubwa kwa bara la Asia na Afrika.

Bwana Yuri Fedotov ambaye ni mkurugezi mkuu wa UNODC amesema dawa zote mbili hutengenezwa kwa ajili ya kupunguza maumivu, hata hivyo wauzaji  kimagendo huzitengeneza na kuzisambaza kinyume na taratibu, hivyo kusababisha madhara makubwa ya afya za mamilioni ya watu duniani kote.

Mwaka 2016 UNODC ilikatama tani 87 za dawa za maumivu zilizopangwa kutumiwa kinyume cha kanuni, kiwango ambacho ni sawa na heroini iliyokamatwa mwaka huo huo.

Bwana Fedotov anasema asilimia 87 ya dawa hizo za maumivu zilikamatwa maeneo ya Afrika ya Kati, Magharibi na Kaskazini.

Amezungumzia pia mihadarati akisema utafiti wa ofisi yake umebaini kuwa soko la madawa na kulevya limezidi kupanuka huku kokeini na bangi vikizalishwa kwa kiwango cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa.

Ameongeza kuwa ripoti hii ni sababu tosha ya jamii ya kimataifa kuongeza jitihada za kimkakati katika  mapambano  dhidi ya uzalishaji, usambazaji na pia matumizi ya mihadarati na matumizi yasiyoruhusiwaya dawa za maumivu.

Katika ripoti hiyo wataalam wamebaini kuwa mihadarati inathiri zaidi vijana  kuliko watu wazima ikitaja barubaru wa kati ya miaka 12  hadi 17 ndio walengwa wakubwa na wakifikia kati ya miaka 18 hadi 25 wanakuwa tayari waathirika wakubwa , umri ambao ni nguvu kazi katika jamii yote ile.

Aidha ripoti imebaini kuwa  vifo vitokanavyo na matumizi ya mihadarati vimeongezeka kwa asilimia 60 kutoka mwaka 2000 hadi 2015.

Matumizi ya mihadarati kwa wanawake imebainika kuwa na athari kubwa kiakili na wengi kati waathirika hao wamekumbwa na unyanyasaji wa kingono katika ukuaji wao.

Ripoti imebaini kuwa idadi ya wanawake wanaopata tiba kutokana na  matumizi ya madawa ya kulevya ni ya juu sana kulinganishwa na wengine.

Kwa mantiki hiyo ripoti inataka tiba ya kukabiliana madawa ya kulevya na VVU ili kuokoa maisha ya wanawake wengi.