Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji bora baharini hutegemea ustawi wa mabaharia-IMO

Meli zikiwa katika bandari ya Antwerp
Picha/ IMO
Meli zikiwa katika bandari ya Antwerp

Usafirishaji bora baharini hutegemea ustawi wa mabaharia-IMO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ustawi  na ufanisi wa shughuli za baharini unategemea  afya  imara na mazingira salama  na endelevu  kwa mabaharia.

Kitack Lim ambaye ni Katibu Mkuu wa shirika la kimataifa la shughuli za majini IMO amesema  hayo katika ujumbe wake wa siku ya mabaharia duniani hii leo,.

Amesema ni katika muktadha huo, shirika hilo linaendelea kuhamasisha jamii ya kimataifa katika kuweka mazingira bora ya ustawi na afya ya mabaharia ili kuwaepusha na matatizo ya kiafya ikiwemo msongo wa mawazo.

Sauti ya Kim

Mabaharia hufanya kazi ngumu mno ambayo inahitaji kuwa makini kiafya na kiakili. Usalama wa kazi ya majini  unategemeana na utaalamu na pia kujitolea kwa mabaharia, licha ya maendeleo ya kisasa katika masuala ya kitekinolojia. Kazi zao zinaweza kuwa na manufaa katika kujipatia kipato ila wakati mwingine ina changamoto nyingi huko baharini ikiwa ni pamoja na likizo fupi,  kuachishwa kazi, migogoro ya malipo ya mishahara na pia walengwa katika uharibifu.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zitatimizwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya usalama wa baharini, ufanisi katika kuzuia na kudhibiti uharibifu wa mazingira utokanao na meli, pamoja na kuzingatia sheria za kimataifa zinazohusiana na ulinzi wa bahari chini ya mkataba wa IMO.

Asilimia 80 ya biashara duniani hutegemea usafirishaji wa majini kupitia meli na hivyo ustawi wa mabaharia ni ustawi wa mbinu hii ya usafirishaji ambayo siyo tu gharama nafuu bali pia ni njia inayotegemea na watu wengi.

Siku ya kimataifa ya mabaharia duniani, huadhimishwa kila 25 mwezi Juni ambapo mwaka huu kaulimbiu ni kuchagiza ustawi wa mabaharia kimwili na kiakili.