Grandi asihi mataifa wahisani kunusuru maeneo ya Afrika yenye migogoro

25 Juni 2018

Kamishina mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi Filippo Grandi, ametoa wito kwa matifa wahisani kusaidia kurejesha utulivu katika nchi za Afrika zilizoghubikwa na migogoro.

Grandi ametoa wito huo alipokuwa katika ziara fupi nchini Mali mwishoni mwa juma na kukutana na mamia ya wakimbizi na wahamiaji mjini Gao, eneo ambalo ni njiapanda ya wasafiri, wahamiaji na wakimbizi lakini pia askari na waasi.

Miongoni mwa wakimbizi walioorodheshwa hapo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, ni zaidi ya 5,000 ambao wamewasili kutoka nchi jirani ya Burkina Faso katika miezi ya karibuni kwenye miji ya mpakani ambako jeshi la serikali lnaipambana na waasi.

 

Kamishina mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi Filippo Grandi akizungumza na wakimbizi wa Nigeria Kaskazini mwa Mali
UNHCR/Jehad Nga
Kamishina mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi Filippo Grandi akizungumza na wakimbizi wa Nigeria Kaskazini mwa Mali

Miongoni mwa wakimbizi hao ni Souaibou Moumouni ambaye amewasili Gao na familia yake, hata hivyo anasema kusaka hifadhi kuna changamoto kwani kwani waasi waliingia mjini hapo na kuchukua watu 50 wenyeji bila kujali wala kutoa sababu, na kwa wakimbizi kama yeye wanahifadhiwa katika vibanda na wengine hawajapata msaada wowote wa chakula hadi sasa.

Wengi wamemsimulia Grandi changamoto zao na ameahidi kuhakikisha wanapata msaada wa UNHCR. Grandi amekuwa Mali baada ya kuzuru Libya na Niger kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ili kuonyesha mshikamano wa UNHCR. Amesema jamii za wenyeji, wakimbizi na wahamiaji walioko Gao wanahitaji utulivu na changamoto kubwa ni rasilimali ‘ hivyo ametoa rai ya mshikamano wa kimataifa kunusuru hali hiyo.

Gao ni maskani ya kituo cha kimataifa cha wanajeshi kutoka nchi 20  wanaounda kikosi cha Umoja wa Mataifa cha ulinzi wa amani ambacho kiko Mali kikifanya kazi ili kurejesha utulivu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter