Haki za wanawake ziko mashakani, tuchukue hatua- Wataalam

22 Juni 2018

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema hatua za haraka zinahitajika  ili kuondokana na tabia inayotishia mafanikio ya haki za wanawake duniani  yaliyopatikana kwa jasho.

Katika ripoti yao waliyowasilisha leo  mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi, wataaalam hao wanaoshughulikia ubaguzi dhidi ya wanawake kisheria na kivitendo wamesema kumekuwa na ongezeko la kuzorota kwa haki za wanawake  katika maeneo mbalimbali ya dunia kutokana na itikadi za kisiasa za upande wa kihafidhi na pamoja na misimamo mikali ya kidini.

Wametaja desturi kama vile kuoa mke zaidi ya mmoja, kuwaoza watoto, ukeketaji na pia kuwachukulia hatua watu kutokana na mwelekeo wao wa kijinsia havina nafasi katika jamii ya leo.

Mambo mengine yanayorudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana ni ongezeko la utawala wa kibabe, migogoro ya kiuchumi na ongezeko la kutokuwa na usawa.

 

Pichani ni walinda amani wawili wanawake ambao ni mafundi gari, Sajini Meseret Adera naKoplo Seblewegel Demesse.
Picha Ya Albert Gonzales Farran
Pichani ni walinda amani wawili wanawake ambao ni mafundi gari, Sajini Meseret Adera naKoplo Seblewegel Demesse.

Wamesema hakuna sababu ya kusubiri kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake na kwamba wakati ni sasa.

Kundi la watalaamu limegusia baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa, likisema kuwa hatua kadhaa zinachukuliwa katika maeneo mbalimbali za kutetea haki za wanawake.

Mafanikio hayo ni pamoja na baadhi ya nchi kuondoa tofauti ya ujira kati ya wanawake na wanaume  pamoja na kuharamisha vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia, ambavyo, kundi linasema ni mafanikio katika vita vya kuondoa ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Wataalamu hao wamesihi jamii ya kimataifa ichukue hatua kuelekea usawa wa kijinsia na kulinda mafanikio hayo yaliyopatikana huku wakipongeza watetezi wa haki za wanawake dunia ambao wamesema wanaendelea na ujasiri wao wa utetezi licha ya vikwazo.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter