Venezuela imeshindwa kuwawajibisha wakiukaji wa haki za binadamu:UN Ripoti

22 Juni 2018

Serikali ya Venezuela imeshindwa kuwawajibisha wakiukaji wa kubwa wa haki za vinadamu ikiwemo mauaji, matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, watu kuswekwa rumande kinyume cha sheria, ukatili na mateso.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi.

Ripoti imeweka wazi athari za ukiukwaji huo katika masuala ya kiuchumi na kijamii hasa kwa haki ya kupata chakula na huduma za afya.

Imeelezea hali ilivyo kwa sasa katika ukiukwaji wa haki za binadamu ulioorodheshwa kenye ripoti ya hali ya haki za binadamu nchini Venezuela ambayo ilitolewa na ofisi ya haki za binadamu mwezi Agost 2017.

Wakati ripoti hiyo ya mwaka jana ilijikita katika matumizi ya nguvu kupita kiasi na mauaji ya kiholela dhidi ya waandamanaji, ripoti hii mpya pia imeorodhesha visa vya kutisha vya mauaji ya kiholela kwa misingi ya operesheni za kupambana na uhalifu zijulikanazo kama “operesheni za ukombozi wa watu” OLPs

 

 

Tangu Julai 2015 hadi Machi 2017 ofisi ya mwanasheria mkuu wakati huo, iliorodhesha mauaji ya watu 505 yaliyotokelezwa na vikosi vya ulinzi wakati wa operesheni hizo.

Ripoti imeongeza kuwa kwa mujibu wa mashahidi upekuzi katika makazi duni ulikuwa kama ada ili kukamata wahalifu bila kuwa na vibali rasmi, mauaji ya vijana , na katika baadhi ya visa vmauaji yalitokea majumbani kwao na hatimaye vikosi vya ulinzi kupindua mazingira ili mauaji yaonekane yalitokea wakati wa majibizano ya risasi.

Ripoti hiyo inasema ushahidi wa waathirika unazusha maswali mengi endapo kweli OLPs zilikuwa na lengo la kutokomeza uhalifu, kwani “kuna dalili zinazoashiria operesheni hizo zilikuwa ni njia ya serikali kuonyesha madai ya kupungua kwa uhalifu”

UNHCR Venezuela/Reynesson Damasc
Wakimbizi wa Venezuela wanaohamishwa kuelekea Brazil.

 

Chini ya mwanasheria mkuu wa zamani maafisa 357 wa usalama walikuwa wanachunguzwa kuhusiana na mauaji lakini tangu wakati huo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa hadharani kuhusu kesi hiyo, kikwazo kikubwa kikiwa ni kitengo cha kisayansi, uhalifu na uchunguzi (CICPC) ambacho ndio chenye jukumu la uchunguzi na ndicho kinachodaiwa kufanya mauaji mengi.

Kwa mujibu wa ripoti mahabusu 39 kwenye kituo cha serikali  jimboni Amazonas wameripotiwa kuuawa mwaka 2017 , na watu 7 wa kundi lenye silaha mjini waliuawa mjini Carcas mwaka 2018 ambako vikosi vya usalama vinadaiwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Ukwepaji sheria pia unaonekana kuwapendelea maafisa wa usalama ambao wadaiwa kukatili maisha ya waandamanaji takriban 46 wakati wa maandamano ya mwaka jana, na mwanasheria mkuu ametoa kibali cha kukamatwa watu 54 lakini hadi sasa ni kesi moja tu ndio iliyoanza kusikilizwa rasmi.

Ushahidi umeelezwa kutoweka kutoka kwenye mafaili, ripoti ikisistiza kwamba “Uongozi wa serikali umeshindwa kuchunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi na mauaji ya waandamanaji yaliyofanywa na vikosi vya ulinzi, na familia za waliopoteza maisha sasa zimepoteza imani na mfumo wa sheria na hazitarajii serikali kuhakikisha uwajibikaji wa aina yoyote”

Helena Carpio/IRIN
Waandamanaji wakiwa La Castellana, mtaa ulioko Mashariki mwa Caracas, Venezuela

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema “Kushindwa kuwajibisha vikosi vya ulinzi kwa makossa hayo makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu kunaonyesha kwamba utawala wa sheria haupo Venezuela, ukwepaji wa sheria ni lazima ukome”

Na kwa sababu Venezuela imekataa kuipa fursa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo licha na maombi kibao, Zeid amependekeza kwamba baraza la haki za binadamu lianzishe tume ya uchunguzi wa hali ya haki Venezuela, na pia kuna kesi nzito ya kuweza kuishirikisha mahakama ya kimataifa ya uhalifu.

Ripoti inasema hali ya kibinadamu ni mbaya familia zinalazimika kusakura chakula majalalani, asilimia 87 ya watu wameathirika na umasikini, huku ufukara ni salimia 61.2 na watu wengine milioni 1.5 wameikimbia nchi tangu 2014.

Sasa Zeid ameitaka serikali na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatuaharaka kuzuia kuzorota Zaidi kwa hali ya kibinadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud