Taasisi imara ni muhimu katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:Guterres

21 Juni 2018

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres,  leo Alhamisi akiwa  mjini Moscow nchini Urusi amesema, kuwa na taasisi imara duniani ni muhimu katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ugaidi na changamoto nyinginezo.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa na serikali ya Urusi zitaendelea kushirikiana  ili kuziweka taasisi za kimataifa kuwa zenye nguvu zaidi na zenye uwezo mkubwa  ili kuweza kusaidia jamii.

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ( wa pili kushoto) akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ( wa pili kushoto) akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov.

Bwana Guterres, akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov, amewaambia waandishi habari mjini Moscow kuwa, “kutokana na changamoto zilizoko, tunahitaji nguvu za pamoja kuweza kuzikabili na hilo linadhihirisha  umuhimu wa taasisi imara za pamoja na uwepo wa sheria zenye muundo wa ushirika wa kimataifa zikiambatana na mkataba wa Umoja wa Mataifa.”

Guterres, ametoa wito huo wakati akihitimisha ziara ya siku mbili nchini humo.

Amewaambia waandishi habari kuwa yeye na wenyeji wake wamejadili changamoto mbalimbali kuanzia Mashariki ya Kati, sehemu kadhaa za Afrika, Korea Kaskazini na Ukraine na pia kugusia migogoro mingine tofauti iliyoko ulimwenguni hivi sasa.

 Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na Urusi zitashirikiana kuhusu mgogoro wa Syria  ambapo amesema lengo ni kuwa na Syria  ambayo mipaka yake inaheshimiwa, na kuweza kujiamulia mustakabali wake na makundi yote kujihisi yanahusishwa.

Katibu Mkuu, akiwa Urusi amekutana na maafisa mbalimbali wa mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa nchini humo na pia mchezaji maarufu wa zamani wa mchezo wa Hockey Vyacheslav Fetisov ambae hivi majuzi aliteuliwa kuwa  mlezi wa ofisi ya mazingira ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Polar.

Pia Katibu Mkuu amekuwa na mazungumzo na rais wa Urusi Vladmir Putin.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter