Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi wanawake wanajenga imani na jamii- Carrilho

Luis Carrilho ambaye ni mshauri wa polisi kwenye Umoja wa Mataifa akihojiwa na Monica Grayley wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
UN News
Luis Carrilho ambaye ni mshauri wa polisi kwenye Umoja wa Mataifa akihojiwa na Monica Grayley wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Polisi wanawake wanajenga imani na jamii- Carrilho

Amani na Usalama

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix ametaka ushirikiano zaidi katika kukabiliana na changamoto zinazokabili shughuli za polisi wa chombo hicho, UNPOL, wanaohudumu kwenye operesheni za ulinzi wa amani.

Bwana Lacroix amesema hayo leo jijini New York, Marekani wakati wa mkutano wa pili wa viongozi waandamizi wa polisi wa Umoja wa Mataifa, UNPOL akisema kukabili changamoto hizo kutazingatia vigezo vya hatua kwa amani, au A4P zilizotangazwa na Katibu Mkuu Antonio Guterres hivi karibuni.

Ametaja mambo muhimu katika vigezo hivyo kuwa ni utashi wa kisiasa, utendaji, ubia, watu, ulinzi wa amani na kuendeleza amani.

Hata hivyo amesema masuala hayo yote yanategemea operesheni za polisi kwa kuwa ndio kiambato kikuu kwenye kusimamia amani, kuendeleza ikiwemo kuhakikisha taasisi za kipolisi za kiserikali zinatekeleza wajibu wao za ulinzi wa ndani.

Image
Polisi wa Umoja wa Mataifa akiwa na watoto. (Picha/UNPolice)

 

Akifafanua majukumu yao ambayo mara nyingi bado hayafahamiki, Luis Carrilho ambaye ni mshauri wa polisi kwenye Umoja wa Mataifa amehojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa na kusema kuwa.

(Sauti ya Luis Carrilho)

 “Kwa ujumla, jukumu letu ni kuweka mazingira ya maisha bora zaidi kwa jamii ambayo tunahudumia, hususan pindi tunapokuwa na operesheni ya ulinzi wa amani tunayohudumia. Kuna makundi ya kuangazia iwe ya kidini, kikabila,kiuchumi,  kisiasa au mengine ambayo yanahitaji kitengo cha polisi cha Umoja wa Mataifa, kichukue hatua. Na maafisa wa polisi wa Umoja wa Mataifa, kutoka nchi wanachama wanahudumia jamii.”

Bwana Carrilho akazungumzia pia umuhimu wa polisi wanawake kwenye operesheni za ulinzi wa amani akisema..

(Sauti ya Luis Carrilho)

“Polisi wa Umoja wa Mataifa wanatokana na polisi ambao wanatoka nchi wanachama, na tunahitaji polisi wengi wanawake kwa sababu kule tunakohudumia, polisi wanawake wanaleta tofauti bora zaidi. Wanahudumia jamii, wanajenga imani kati ya polisi na jamii kwa sababu polisi huhudumia jamii. Na ninaamini tukiwa na idadi kubwa zaidi ya polisi wanawake tutakuwa katika tumejiandaa vyema zaidi kupatia ulinzi jamii tunazohudumia.”